1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msichana wa pili wa Chibok apatikana

20 Mei 2016

Msichana wa pili wa Chibok ameokolewa, jeshi la Nigeria limesema, baada ya rais Buhari kukutana na msichana wa kwanza mwanafunzi aliyeokolewa na kueleza matumaini ya kupatikana wasichana wengine.

https://p.dw.com/p/1Ir30
Nigeria Zweites Chibok Girl befreit
Msichana wa pili wa Chibok kuokolewa na jeshi la NigeriaPicha: Reuters

Zaidi ya wasichana wengine 200 bado wanashikiliwa na kundi la Boko Haram.

Katika taarifa fupi Alhamisi saa chache baada ya rais Muhammadu Buhari kukutana na mwanafunzi Amina Ali katika mji mkuu Abuja, msemaji wa jeshi kanali Sani Usman, alithibitisha kuokolewa kwa msichana mwingine wa Chibok. Maelezo zaidi kuhusu msichana huyo wa pili yatatolewa baadaye amesema msemaji huyo wa jeshi.

Nigeria Präsident Buhari empfängt befreites Schulmädchen Amina Ali
Rais Buhari akizungumza na msichana wa kwanza kuokolewa Amina AliPicha: Getty Images/AFP/Stringer

Amina mwenye umri wa miaka 19, ambaye ana mtoto mchanga wa kike, aligunduliwa na walinzi wa kijamii na wanajeshi siku ya Jumanne na alisafirishwa pamoja na mama yake Binta kukutana na rais katika makaazi yake rasmi ya Aso Rock.

Buhari amesema amefurahishwa kwa kuachiliwa huru na serikali inafanya kila inachoweza kuweza kuachiwa wasichana wengine waliobaki wa Chibok, ambao walitekwa kutoka katika mji huo kaskazini mashariki mwa Nigeria Aprili 14, 2014.

"Kuokolewa kwa Amina kunatupa matumaini, na kunatoa fursa adimu kwa kupata taarifa muhimu," ameongeza rais Buhari.

BringBackOurGirls Nigeria Geisel Boko Haram
Wanaharakati wakikumbatiana katika tukio la kukaa mjini Abuja wakidai kuchukuliwa hatua kuwaokoa wasichana waliotekwaPicha: Reuters/A.Sotunde

"Licha ya kwamba hatuwezi kufanya chochote kuondoa hali ya kutisha aliyonayo, serikali kuu inaweza na itafanya kila kinachowezekana kuhakikisha kwamba maisha yake yanachukua mkondo tofauti kabisa."

Jumla ya wasichana 276 walitekwa nyara kutoka katika shule ya sekondari ya serikali ya wasichana, ambapo 57 walifanikiwa kutoroka katika saa chache baada ya kutekwa.

"Warudisheni wasichana wetu"

Utekaji huo ulizusha hasira kubwa duniani na kusababisha mzozo huo kuhusisha watu wengi duniani lakini hadi Amina na msichana mwingine walipopatikana, kulikuwa na ishara chache juu ya uwezekano wa kuachiwa.

Hadiza Bala Usman ni mwanaharakati anayeongoza kampeni maarufu kama, "warudisheni wasichana wetu" amesema amefurahishwa sana kuwaona wasichana hao wawili.

Nigeria Bildergalerie Staatspräsidenten Goodluck Jonathan
Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck JonathanPicha: T. Charlier/AFP/Getty Images

"Nina furaha sana, nina wasiwasi pia, kuna wasiwasi mkubwa kuhusu wasichana wengine na hali waliyonayo, lakini pia inaonesha kwamba kuna hali ya ongezeko la mapambano katika kuwatafuta."

Wasichana hao waliotekwa walikuwa kwa muda mrefu wakifikiriwa kuwa wamepelekwa msituni. Picha za satalaiti zilizotolewa na Marekani na Uingereza zinaripotiwa kutambua mahali baadhi ya wasichana hao walipo.

Lakini jeshi la Nigeria lilishindwa kuchukua hatua kutokana na taarifa hizo za kijasusi, amedai balozi wa zamani wa Uingereza nchini Nigeria.

Nigeria Eine der durch Boko Haram verschleppten Schülerinnen ist frei
Picha ya kwanza iliyotolewa na jeshi la Nigeria ya Amina AliPicha: picture-alliance/dpa/Nigerian Military

Kuchelewa kwa rais wa zamani Goodluck Jonathan kuchukua hatua kuhusiana na utekaji huo pamoja na jinsi alivyolishughulikia kwa jumla suala la wapiganaji kumeonekana kuwa sababu kuu katika kushindwa kwake na Buhari katika uchaguzi mwaka jana.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Josephat Charo