1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msimamo wa Umoja wa Ulaya kutokana na kukamatwa kwa Radovan Karadzic

Othman, Miraji22 Julai 2008

Kukamatwa kwa Radovan Karadzic kumepokelewa kwa uzuri kote duniani.

https://p.dw.com/p/EhrW
Picha ya Radovan Karadzic, kiongozi wa zamani wa Waserbia wa Bosnia, baada ya kukamatwa mjini BelgradePicha: AP


Na kama alivosema leo waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa na rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Bernard Kouchner, katika mkutano wa mawaziri wa Umoja huo mjini Brussels, ni kwamba tokeo hilo wamelingojea kwa miaka 13.

"Hamna idara yeyote rasmi ya Serbia inayojua wapi waliko Karadzic na Mladic", hayo ni maneno yaliotamkwa wiki iliopita na waziri wa Serbia ambaye ana dhamana ya kushirikiana na Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ilioko The Hague, Uholanzi. Muda mfupi baadae mtu anayeshukiwa kuwa ni mhalifu wa kivita anayetafutwa sana, kwa udi na uvumba, alikamatwa katika kiunga cha mji mkuu wa Belgrade. Na kwa mujibu wa habari za mwanzo alikamatwa akiwa katika basi la kawaida la abiria. Zile tetesi, kwa mfano, kwamba Radovan Karadzic alijificha mahala fulani huko Russia, au kwamba alifanya operesheni ya uso ili asiweze kutambuliwa, zote hizo zimedhihiri kuwa ni upuuzi mtupu. Tetesi hizo zilikuwa sehemu ya mbinu za makusudi za serekali ya zamani ya Serbia, chini ya uongozi wa Vojislav Kostunica, kuwababaisha watu.

Kukamatwa Radovan Karadzic kumeonesha kwamba mbinyo uliowekwa na Umoja wa Ulaya kwa Serbia ulikuwa sawa. Mbinyo huo unafaa uendelezwe hadi pale yule jenerali wa Karadzic, yaani Ratko Mladic, na kiongozi wa Wa-Serbia wa Kroatia, Goran Hadzic, nao waonekane katika mahabusi ya Mahakama ya Umoja wa Mataifa huko The Hague. Hapo kabla,si nchi zote za Umoja wa Ulaya zilizokuwa kakamavu pale lilipokuja suala la kutoregeza kamba hata kidogo katika kutaka kuwakamata wale watu wote wanaoshtakiwa kuendesha uhalifu wa kivita huko Bosnia, na kulifanya jambo hilo kama sharti kwa Serbia kukaribiana na Umoja wa Ulaya. Ni Ubelgiji na Uholanzi tu zilizokataa kutekelezwa yale mapatano yaliokwishatiwa saini na Serbia. Tutarajie kwamba nchi hizo zitasimama kidete na kutaka, kama ilivokuwa kabla, kwamba washukiwa wote wa uhalifu wa kivita lazima wapelekwe mbele ya Mahakama ya The Hague.

Pia jamii ya kimataifa lazima iiunge mkono kikweli serekali ya Serbia. Hatua hiyo ya mshangao ya kukamatwa Radovan Karadzic ni ya kijasiri. Lakini licha ya sifa zote hizo, tusisahau kwamba kunahitaji kuchukuliwa hatua mbili muhimu kufikia kwenye lengo. Na tu ikiwa hatua hizo zitachuliwa ndipo ule ukurasa wa kiza wa historia ya karibuni ya Serbia utakapofungwa. Jambo hilo sio tu muhimu kwa Serbia. Katika nchi jirani ya Bosnia-Herzegovina wanangoja jamaa za familia zilizokuwa wahanga wa wauaji waliongozwa na Karadzic; Jamaa wa wahanga hao wananngoja kuona haki inatendwa. Kwa mama wa watu waliouliwa huko Srebrenica, kukamatwa kwa Radovan Karadzic hakutarejesha maisha ya watoto na waume zao. Lakini ile hisia kwamba haki, baada ya kupita muda mrefu, imeshinda, bila ya shaka, itasaidia kufanya mzigo wa machungu wanayoyabeba kuwa mwepesi kidogo. Katika eneo la Balkan kulitapakaa tetesi kwa miaka kwamba kulifanywa makubaliano na Karadzic, kwamba ajitoe kutoka siasa na badala yake atahakikshiwa uhuru, kutokamatwa. Lakini sasa kwamba amekamatwa, jambo hilo litawarejeshea familia za wahanga wa huko Bosnia ile imani walioipoteza kwa kile kinachoitwa jamii ya kimataifa, japokuwa kuna watu wengi wanasema mapatano kama hayo huenda yalikuweko.

Sasa Radovan Karadzic, daktari wa magonjwa ya akili, atatakiwa aelezee ukweli wote, na jambo hilo litasaidia kuvichambua Vita vya Balkan, licha kwamba watu wengi hawatapenda ifanywe hivyo.