1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msumbiji yatangaza tarehe ya uchaguzi wake mkuu

30 Aprili 2009

Guebuza na Dhlakhama katika Urais

https://p.dw.com/p/Hhaw
Rais wa sasa Armando Guebuza .Picha: picture-alliance/dpa

Msumbiji imepanga tarehe 28 Oktoba kuwa tarehe ya uchaguzi mkuu, ambao wachambuzi wanasema utaashiria mwisho wa chama cha Renamo cha waasi wa zamani Renamo, kuwa chama cha upinzani cha kutegemewa katika taifa hilo la demokrasia changa.

Chama hicho cha Renamo kilishindwa katika chaguzi za mameya mwaka jana na sasa kinakabiliwa na kitisho cha kupoteza nafasi yake kama chama kikuu cha upinzani kwa chama cha Democratic-MDM kilichoundwa na wanasiasa waliojitenga na Renamo

Wachambuzi wanasema chama cha Frelimo kikijiandaa kunyakua ushindi mwengine, angalau chama kimoja cha upinzani kinapaswa kupata uungaji mkono wa kutosha kuzuwia uwezekano wa taifa hilo kurudi katika mtindo wa miaka ya nyuma ya siasa kudhibitiwa na chama kimoja , jambo ambalo lilikua chanzo cha kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka 16 nchini Msumbiji.

Afisa kutoka taasisi ya uchaguzi kusini mwa Afrika(EISA) Miguel de Brito anasema ikiwa chama cha MDM kitashindwa kupata uungaji mkono wa kutosha katika uchaguzi huo ujao na kuwa na uakilishi bungeni na kama Renamo nayo itapata matokeo sawa na ya uchaguzi wa serikali za mitaa, basi kuna hatari ya kurudi katika mfumo wa chama kimoja.

Renamo inapongezwa kwa kupigania mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini Msumbiji, ambapo ilipigana vita na Frelimo kilichokua wakati huo chama cha Kimarxisti, baada ya uhuru kutoka kawa Ureno 1975.

Lakini sasa Renamo imo mbioni kujaribu kuondoa sura yake ya zamani kama jeshi la wapiganaji wa chini kwa chini waliopigana vita wakisaidiwa na utawala wa wazungu wachache wa iliokua Rhodesia ambayo sasa ni Zimbabwe na utawala wa wazungu wa kibaguzi nchini Afrika kusini.

Baada ya kusainiwa mkataba wa amani 1992, Renamo kilishindwa kugeuza uasi wake kuwa mafanikio katika uchaguzi. Kiongozi wa chama hicho Afonso Dhlakama amepigania urais mara tatu biala mafanikio na Renamo hakijapata kupata wingi wa kura bungeni.

katika uchaguzi uliopita 2004, muungano wa Renamo ulipata asili mia 30 tu ya kura. Dhlakama akashindwa katika uchaguzi wa rais na Armando Guebuza.

Uchaguzi wa safari hii utakua sawa na marudio ya ushindani kati ya Guebuza na Dhlakama, ambapo wote wameshaidhinishwa na vyama vyao kuwa wagombea.

Huenda uchaguzi huo ukamjumuisha pia Daviz Simango, aliyepata umaarufu kitaifa baada ya kujiengua kutoka Renamo na kuunda chama kipya cha Democratic MDM.

Kwa ushindi huo Simango ni meya pekee asiyetoka chama cha Frelimo nchini Msumbiji.

Wachambuzi wanaashiria kwamba MDM kinaweza kusababisha sura mpya ya kisiasa nchini humo, katika wakati ambao mamlaka makubwa ya Frelimo yamezidisha ile hali ya kutokuwepo na usawa nchini humo.

Lakini hayo kwa sehemu kubwa yatategemea idadi ya wapiaga kura watakaojitokeza katika uchaguzi wa Oktoba.Katika uchaguzi wa rais 2004 ni asili mia 36 tu ya wapiga kura walioshiriki kutoka asili mia 70 mwaka 1999 na asili mia 80 , katika mwaka 1994.

Kwa hivyo kushiriki kwa idadi kubawa ya wapiga kura ni muhimu ili kutoa ushindani wa kweli wa kidemokrasi nchini Msumbiji.

Kwa kuzingatia yote hayo kwa hivyo, siri kubwa ya chama chochote , ambayo hakuna aliyefanikiwa kuigundua bado , ni jinsi gani ya kuwashawishi asili mia 50 iliosalia ya wapiga kura ambao hawakushiriki katika uchaguzi uliopita, waweze kuitumia haki yao ya kikatiba na kushiriki katika uchaguzi mkuu wa tarehe 28 Oktoba.

Mwandishi: Mohamed AbdulRahman/AFPE

Mhariri:O.Hamidou