1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtanzania kukabidhiwa tuzo Ujerumani

Saumu Mwasimba
27 Novemba 2018

Mwanaharakati wa mazingira Gerald Bugurube kutoka Tanzania na Clovis Razafimalala wanakabidhiwa tuzo ya Ujerumani kwa Afrika kutokana na juhudi zao za kutunza maliasili za nchi zao

https://p.dw.com/p/38zgD
Deutsche Afrika Stiftung Pressebild | Gerald Bigurube & Detlef Wächter
Picha: Deutsche Afrika Stiftung

Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika (German Africa Award) inayotolewa kila mwaka kwa watu walioonyesha mfano katika sekta ya kutunza mazingira, mwaka huu imewaendea Gerald Bigurube kutoka Tanzania na Clovis Razafimalala wa Madagascar. Watu hao wawili wamesifiwa kwa kujitolea kunusuru maliasili katika nchi zao. Wanaharakati hao wa mazingira wanakabidhiwa tuzo hiyo  leo 26.11.2018 hapa Ujerumani.

Kwa miaka 44, Gerald Bigurube, Mtanzania mwenye umri wa miaka 66 amejitolea maisha yake kuwaokoa wanyama wa porini pamoja na mazingira asilia nchini mwake. Kwa muda mrefu amekuwa mkuu wa Mamlaka ya hifadhi za  Taifa za Wanyama pori Tanzania, TANAPA aliongoza mapambano dhidi ya majangili, na alianzisha juhudi za ujirani mwema baina ya mamlaka za kuhifadhi wanyamapori na jamii zinazoishi karibu na mbuga, pamoja na utalii ambao ni mojawapo ya nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania.

Kwa upande wa Mmalagasi Clovis Razafimalala ambaye ana umri wa miaka 46, ingawa amekuwa katika harakati za kutunza mazingira kwa muda mfupi zaidi, juhudi zake zimejikita katika kuulinda msitu wa asili katika nchi yake ya kisiwa. Kama mkuu wa Shirika la Maroantsetra Lampogno, Razafimalala amejitosa katika vita dhidi ukataji haramu na usafirishaji wa magogo na mbao, hususan katika eneo la Mbuga ya Wanyama ya Masoala, ambayo imewekwa kwenye orodha ya turathi za dunia ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni - UNESCO.

Deutsche Afrika Stiftung Pressebild | Clovis Razafimalala & Marcus Schneider
Picha: Deutsche Afrika Stiftung

Ukataji haramu wa magogo umekithiri sambamba na ufisadi baada ya mzozo wa kisiasa ulioanza kisiwani  Madagascar mwaka 2009, ambao ulianza na maandamano dhidi ya serikali ya kidikteta. Mwaka 2016, Mwanaharakati huyo alikamatwa na serikali na kuwekwa kizuizini, kwa tuhuma za kuongoza maandamano dhidi ya makampuni ya mbao, licha ya kwamba wakati wa maandamano yanayotajwa hakuwepo. Kabla ya tukio hilo, alikuwa amefichua njama ya serikali ya mkoa na wafanyabiashara wenye nguvu  kuruhusu usafirishwaji wa mbao za mti wa liwa,kwenda China.

Akizungumzia kuchaguliwa kwa Bigurube na Razafimalala, Katibu Mkuu wa Wakfu wa German Africa, Ingo Badoreck, amesema jopo huru la watu 26 limeamua kuwa muda umefika kuwapa sauti wanaharakati ambao wametoa mchango katika kulinda mazingira.

Tukinukuu maneno ya Badoreck amesema ''Tunataka kuthibitisha kwamba maendeleo ya kiuchumi huenda sambamba na utunzaji wa mazingira.''

Pamoja na kwamba Razafimalala amejulikana kupitia vuguvugu la wanaharakati wa mashinani, wakati mafanikio ya Bigurube yamekuja akiwa ni  mtumishi wa serikali, wote wawili wamefanya juhudi kwa ushirikiano na serikali, kuondoa kero za kimazingira.

''Razafimalala aliiweka wazi mitandao inayoratibu usafirishaji nje wa mbao za miti ya liwa,'' amesema Badoreck. Kuwekwa kwake kizuizini kulifuatiliwa kwa karibu na mashirika ya kutetea haki za binadamu, kama vile Amnesty International, ambayo yalipigania kuachiwa kwake.

Badoreck amesema leo hii nchini Madagascar wapo maofisa wa serikali ambao wanaunga mkono juhudi za kutunza mazingira. Amesema kama wanavyoonyesha Clovis Razafimalala na Gerald Bigurube, bila shaka ushirikiano na serikali unahitajika kuweza kufanikiwa katika shughuli za kuyalinda mazingira.

Katibu Mkuu Wakfu wa German Africa amemsifu Bigurube kwa kuweka mkakati wa namna utunzaji wa mazingira na ukuaji wa uchumi, vinavyoweza kusaidiana.

Tanzania yenye vivutio maarufu vya watalii, kama Kreta ya Ngorongoro na mbuga za wanyama kama Serengeti, ina sifa ya kuwa na hifadhi nzuri ambazo ni takribani asilimia 40 ya eneo la nchi nzima. Lakini hata huko, utengamano kati ya hifadhi hizo na shughuli za uchumi unakabiliwa na changamoto.

Tansania Selous Reservat
Mbuga ya wanyama pori ya Selous nchini TanzaniaPicha: WWF Deutschland/Astrid Dill

Kwa wakati huu hifadhi ya Selous ambayo ni miongoni mwa zilizo kubwa zaidi barani Afrika inakabiliwa na shinikizo kubwa. Kuna mpango wa kujenga bwawa kubwa la umeme katika mbuga hiyo, na Gerald Bigurube ni mmoja wa watu ambao wanapaza sauti kusema, ''hebu kwanza tuzungumzie faida za hifadhi hii, kabla ya kuchukua hatua ambazo haziwezi kubadilishwa.''

Akizungumza na DW baada ya kutangazwa mshindi wa tuzo ya German Africa,mwezi Mei mwaka huu,  kuhusu kutangazwa hivi karibuni kwa zabuni za kukata magogo katika mbuga ya Selous, Bigurube alisema kwa vile tayari uamuzi umekwishachukuliwa na serikali, kilichobaki ni kuangalia namna athari za kimazingira zitokanazo na ukataji huo zinavyoweza kudhibitiwa.

Washindi wa awali wa Tuzo hii ya Ujerumani kwa Afrika  ni pamoja na mwanasheria mtetezi wa haki za binadamu nchini Uganda Nocolas Opiyo, mtetezi wa haki za kijamii nchini Afrika Kusini Thuli Madonsela. Wengine ni mwanaharakati wa vyama vya wafanyakazi nchini Tunisia Houcine Abassiand, na mtunzaji wa nyaraka za kihistoria za  Timbuktu Abdel Kader Haidara.

Tuzo hiyo inawapa walioipokea kutambuliwa kimataifa, na pia huwapa jukwaa la kuendeleza harakati zao.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed AbdulRahman

http://www.dw.com/en/conservationists-honored-with-german-africa-award/a-43883054