1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtoto wa miaka 16 anaweza kuoa ama kuolewa Jordan

Lilian Mtono
8 Aprili 2019

Bunge la Jordan leo Jumatatu (08.04.2019) limeifanyia mabadiliko sheria ya ndoa itakayowaruhusu majaji katika kesi "zisizokuwa za kawaida" kuruhusu ndoa za watoto kuanzia umri wa miaka 16.

https://p.dw.com/p/3GTLA
The everyday reality of refugees around the world
Picha: Denis Bosnic

Hili ni ongezeko la mwaka mmoja kutoka umri wa hapo awali wa miaka 15.

Mabadiliko hayo yamepitishwa na mabunge yote mawili ya wawakilishi na baraza la seneti.

Umri wa chini wa mtu kuolewa ama kuoa katika mazingira ya kawaida nchini humo ni miaka 18, lakini mahusiano yanayohusisha watoto yanaweza yakapewa upendeleo na majaji, ali mradi tu wawe wamekidhi masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na ridhaa ya msichana juu ya ndoa hiyo. 

Hata hivyo sheria hiyo inapitishwa wakati makundi ya haki za wanawake ya Jordan kwa muda mrefu yakiwa yanapiga kampeni dhidi ya ndoa hizo za utotoni.

Wiki iliyopita, shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, HRW lililiomba bunge la Jordan kukataza mila hiyo wakisisitiza kwamba wasichana ndio wamekuwa waathirika wakubwa tofauti na ilivyo kwa wavulana. 

"Jordan inatakiwa kutumia fursa iliyonayo kuzuia ndoa za utotoni na kutekeleza sheria inayosema umri wa ndoa ni miaka 18 tena bila ya kubagua,'' lilisema kundi hilo la HRW.

Kaimu mkurugenzi wa HRW kanda ya Mashariki ya Kati, Michael Page amesema ndoa za utotoni zinawazuia watoto kuufaidi utoto wao na kuziweka mashakani afya na hata fursa zao za kielimu.

Kulingana na wizara ya sheria, kulifungwa ndoa 77,700 nchini Jordan mnamo mwaka 2017 na miongoni mwake, kesi 10,434 ambazo ni sawa na asilimia 13.4 zilihusisha msichana wa chini ya miaka 18.