1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtuhumiwa wa mashambulizi ya mjini Brussels akamatwa

9 Aprili 2016

Mtuhumiwa wa shambulio la mjini Paris Mohamed Abrini amekamatwa pamoja na watu wengine wanne katika misako iliyofanyika jana Ijumaa(08.04.2016)wakihusishwa na shambulio dhidi ya uwanja wa ndege wa mjini Brussels.

https://p.dw.com/p/1ISNZ
Mtuhumiwa wa mashambulizi mjini Brussels Mohamed Abrini

Kukamatwa kwa watu hao kunaashiria hatua muhimu katika uchunguzi kuhusiana na kundi linaloaminika kuwa limefanya mashambulio ya tarehe 13 Novemba ambayo yamesababisha watu 130 kuuwawa mjini Paris na Machi 22 ambapo watu 32 waliuwawa mjini Brussels.

Katika mashambulizi hayo yote kundi la Dola la Kiislamu lililoko nchini Iraq na Syria lilidai kuhusika na kutoa ishara ya hali ya hatari katika mataifa ya Ulaya.

Watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na Mohammed Abrini, ambae amekuwa mtu anayetafutwa kimataifa tangu Novemba, baada ya polisi kupata video ambamo anaonekana akiendesha gari ambayo baadaye ilitumika katika mashambulizi mjini Paris.

Waendesha mashitaka wamethibitisha jana Ijumaa(08.04.2016)kwamba wamegundua alama za vidole za Abrini na vinasaba vya DNA katika gari hiyo , pamoja na anuani mbili mjini Brussels zinazohusishwa na mashambulizi ya mjini Paris na Brussels.

Festnahme des Terrorverdächtigen Abrini
Mohamed Abrini akikamatwa na polisi wa UbelgijiPicha: Reuters/S. Dana-Kamran

Kufuatia kukamatwa kwa Abrini , vyombo vya habari vya Ubelgiji vimeripoti kwamba huenda ni mshambuliaji aliyekimbia baada ya shambulio la uwanja wa ndege wa Brussels Machi 22, akiacha kitu cha kuripuka.

Ni mapema mno

Lakini waendesha mashitaka wamesema ni mapema mno kusema iwapo wamemkamata mtuhumiwa ambaye alikuja kufahamika kama mtu mwenye kofia, kwa misingi ya video iliyopatikana.

Siku ya Alhamis, mwendesha mashitaka wa Ubelgiji aliomba umma kusaidia katika kukusanya ushahidi zaidi kuhusu mtu huyo.

Festnahme des Terrorverdächtigen Abrini
Mohamed Abrini alipokamatwa na polisi wa UbelgijiPicha: Reuters/S. Dana-Kamran

Watu hao waliokamatwa siku ya Ijumaa ni pamoja na mtu aliyetambuliwa kuwa Osama K, wamesema waendesha mashitaka.

Baraza la usalama la taifa

Alikamatwa katika mji wa Ulm nchini Ujerumani na kupelekwa nchini Ubelgiji Oktoba 3 katika gari ya kukodi iliyokodiwa na Abdeslam.

Belgien höchste Terrorwarnstufe in Brüssel - Premierminister Charles Michel
Waziri mkuu wa Ubelgiji Charles MichelPicha: Reuters/F. Lenoir

Baraza la taifa la usalama nchini Ubelgiji linatarajiwa kukutana leo Jumamosi (09.04.2016), kufuatia kukamatwa kwa watu wengine zaidi kuhusiana na mashambulizi ya mjini Brussels.

Kikao hicho cha baraza la taifa la Usalama kitahudhuria pia na waziri mkuu Charles Michel, mkuu wa polisi na huduma za upelelezi, pamoja na kitengo cha uratibu cha nchi hiyo kinachofanya tathmini juu ya vitisho vya ugaidi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dfpae / afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid