1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtuhumiwa wa miripuko ya Boston atiwa mbaroni

20 Aprili 2013

Mshukiwa wa mwisho katika utegaji wa mabomu yaliyowauwa watu 3 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 180 katika mbio za Marathon za Boston amekamatwa akiwa ndani ya boti. Polisi imesema kuwa amepelekwa hospitali akiwa mahututi.

https://p.dw.com/p/18Jlb
Polisi wa kupambana na ugaidi mjini Boston wakiwa kazini
Polisi wa kupambana na ugaidi mjini Boston wakiwa kaziniPicha: reuters

Kukamatwa kwa mtu huyo Dzhokhar Tsarnaev, mwenye umri wa miaka 19 kumehitimisha operesheni kubwa ya siku nne, na kumekuja siku moja baada ya shirika la upelelezi la Marekani FBI kuchapisha picha za washukiwa hao. Mshukiwa mwingine, Tamerlan Tsarnaev mwenye umri wa miaka 26 na ambaye ni kaka wa Dzhokhar, aliuawa jana Ijumaa katika majibizano ya risasi na polisi.

Umati wa watu katika mji wa Boston ulishangilia kwa shangwe baada ya kuibuka kwa ripoti ya kukamatwa kwa mshukiwa huyo. Shughuli zote katika mji huo zilikuwa zimesimamishwa wakati operesheni ya kuwasaka vijana hao ilipokuwa ikiendelea.

Kaka waripuaji: Tamerlan Tsarnaev (Kushoto) na mdogo wake Dzhokhar
Kaka waripuaji: Tamerlan Tsarnaev (Kushoto) na mdogo wake DzhokharPicha: picture alliance/AP Photo

Bado yapo maswali yasio na majibu

Akizungumza muda mfupi baada ya kukamatwa kwa Dzhokhar Tsarnaev, rais wa Marekani Barack Obama alisema kukamatwa kwa mshukiwa huyo ilikuwa hatua muhimu katika mkasa unaohusu miripuko ya Boston. Hata hivyo, Obama alisema kuwa bado yanabakia maswali yasio na majibu, ambayo ni pamoja na sababu iliyowafanya vijana hao kufanya mashambulizi, na ikiwa walikuwa na msaada katika uhalifu wao.

''Tutatathmini kilichotokea, na tutachunguza kama magaidi hawa walikuwa na washirika, na tutafanya chochote kinachohitajika kuhakikisha usalama wa watu'', alisema rais Obama.

Mripuko kwenye mbio za Marathon za Boston iliuwa watu 3 na kujeruhi zaidi ya 180
Mripuko kwenye mbio za Marathon za Boston iliuwa watu 3 na kujeruhi zaidi ya 180Picha: picture-alliance/AP

Polisi mjini Boston wamesema kuwa watu wengine watatu wamekamatwa na wanahojiwa kwenye nyumba aliyoishi Dzhokhar Tsarnaev karibu na chuo kikuu cha Massachusetts.

Polisi wamesema walikuwa wakianza kukata tamaa katika operesheni yao, hadi pale walipopigiwa simu na raia ambaye ameiona damu kwenye boti yake, na kumkuta mshukiwa ndani ya boti hiyo akiwa ametokwa na damu nyingi.

Hisia kali dhidi ya Marekani

Watuhumiwa hao wametambuliwa kuwa ni jamii ya Chechen kutoka kusini mwa Urusi, ambao inaaminiwa wamekuwa wakiishi Marekani kwa muda wa miaka 10. Jimbo la Chechnya limeshuhudia vita viwili vikubwa tangu mwaka 1994, baina ya Urusi na wapiganaji wanaotaka kujitenga kwa jimbo hilo.

Kaka mkubwa Tamerlan anasemakana alikuwa na maoni makali dhidi ya Marekani, akiishutumu nchi hiyo kutumia Biblia kama kisingizio kuzivamia nchi nyingine.

Kabla ya kukamatwa kwa mdogo wake mji wa Boston ulikuwa umepooza, baada ya utawala kufunga barabara zote na kuwashauri wenye biashara kuzifunga. Hali kadhalika wakazi milioni moja wa mji huo na vitongoji vyake walikuwa wameombwa kubakia ndani ya nyumba zao, na kufungua mlango tu kwa maafisa wa polisi waliovalia sare.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/RTRE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo