1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtuhumiwa wa ugaidi kubakia katika jela ya Guantanamo

Tuma Provian Dandi10 Oktoba 2007

Mahakama ya mjini Columbia nchini Marekani imepinga hatua ya kutaka kurejeshwa nyumbani kwa mtuhumiwa mmoja wa ugaidi raia Tunisia

https://p.dw.com/p/C77u
Baadhi ya wafungwa katika gereza la Guantanamo
Baadhi ya wafungwa katika gereza la GuantanamoPicha: AP

Jaji Gladys Kessler wa Mahakama ya Kuu ya Columbia amefikia uamzi huo baada ya serikali ya Marekani kutaka kumrejesha nchini Tunisia Bwana Mohammed Abdul Rahman, anayetuhumiwa kwa vitendo vya ugaidi.

Jaji Kessler amesema ikiwa mtuhumiwa huyo atarejeshwa kwao nchini Tunisia, kuna kila uwezekano wa kutendewa madhara mabaya, badala yake mahakama ikatoa amri ya kubakia katika gereza la Guantanamo.

Kwa kipindi kirefu Marekani imekuwa ikifikiria kulifunga gereza la Guantanamo linalohifadha watuhumiwa wa matendo ya ugaidi kutoka sehemu tofauti duniani, lakini nchi wanazotoka watuhumiwa hao zimekuwa zikikataa kuwapokea kutokana sababu mbalimbali.

Hata hivyo tayari Marekani imeshawapeleka nchini mwao zaidi ya wafungwa 450 wanaohusishwa na vitendo vya kigaidi, ili kupata hukumu au kutumikia vifungo vyao, huku gereza hilo la Guantanamo likibaki na kiasi cha wafungwa 330.

Kurudishwa kwa baadhi ya watuhumiwa nchini mwao kunatokana na sababu nyingi ikiwemo kutokuwa na ushahidi kamili juu ya mtuhimiwa, baada ya kukaa kifungoni kwa kipindi kirefu bila kusomewa mashtaka.

Kitendo cha kushikiliwa kwa muda mrefu bila kusomewa mashtaka pia kimekuwa kikipingwa na baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa kuwa watuhumiwa wengine hushikiliwa gerezani bila kufanya makosa ya kigaidi.

Akimtetea mteja wake mahakamani, wakili wa Bwana Mohammed Abdul Rahman, ameitaka mahakama hiyo ya Columbia kutomrejesha mtuhumiwa huyo nyumbani kwao Tunisia, kwa madai kwamba serikali ya nchi hiyo inaweza kumfanyia vitendo vibaya zaidi, badala yake ni bora aendee kuwemo katika gereza la Guantanamo.

Tunisia inasemekana kutozingatia haki za binadamu.

Akishikiliwa kwa miaka kadhaa katika gereza la Guantanamo lililoko katika kisiwa cha Cuba, tayari Bwana Mohamed Abdul Rahman alikuwa meshahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na serikali ya Tunisia.

Akithibitisha kwa kauli yake, mfungwa huyo raia wa Tunisia amesema yuko tayari kubakia mikononi mwa magereza ya Marekani, kuliko kurejea nyumbani ambako anajua kwamba atapata mateso makubwa na suluba nyingi.

Wafungwa kadhaa wa Tunisia waliorejeshwa kutumikia vifungo vyao nyumbani, wanasemekana kupata mateso makubwa kuliko walipokuwa wakishikiliwa katika gereza la Guantanamo.

Wakati mahakama Kuu ya Columbia nchini Marekani ikitoa uamzi wake dhidi ya raia huyo wa Tunisia kubakia katika gereza la Guantanamo, imetupilia mbali rufaa ya raia mmoja wa Ujerumani mwenye asili ya Lebanon, aliyetaka kulishitaki shirika la Kijasusi la Marekani-CIA, kwa kumdhalilisha na kumtesa.

CIA ilimshikilia raia huyo anayeitwa Khaled El Masri katika gereza la Afghanistan na baadaye kumwachia baada ya kukosa ushahidi. Kukataliwa kwa rufaa yake pia kunahusishwa na kuweka hadharani kwa baadhi ya siri za serikali ya Marekani.

Bwana El Masri alikamatwa na CIA nchin Macedonia na kushikiliwa katika gereza la Afghanistan, baadaye akahamishiwa katika jela ya Albania ambapo alishikiliwa kwa miezi mitano baadaye akaachiwa huru kwa madai kwamba alikamatwa kimakosa.