1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mubarak aahidi kupandisha mishahara

8 Februari 2011

Rais wa Misri Hosni Mubarak ameendelea kuvuta muda akiwa madarakani, wakati maandamano ya mitaani yakiendelea mjini Cairo na miji mingine ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/10CkV
Rais Hosni Mubarak wa MisriPicha: picture-alliance/dpa

Rais wa Misri Hosni Mubarak anajaribu kuvuta muda akiwa madarakani , wakati maandamano ya mitaani yakiendelea , mjini Cairo na miji mingine ya nchi hiyo. Mubarak ameahidi kupandisha mishahara ya sekta ya umma kwa asilimia 15 na kuamuru ufanyike uchunguzi kuhusiana na ghasia zilizosababisha umwagikaji wa damu. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 alikutana kwa mara ya kwanza jana na baraza lake jipya la mawaziri.

Ägypten Proteste auf dem Tahrir Platz in Kairo
Waandamanaji nchini Misri wakiwa katika uwanja wa TahrirPicha: picture-alliance/dpa

Waandamanaji nchini Misri wameendelea kujikusanya katika eneo la Tahrir mjini Cairo leo huku kukiwa na miito mipya ya kufanya maandamano nchi nzima kuadhimisha wiki mbili za maandamano ya kuipinga serikali. Mamia kadha ya waandamanaji tayari wanaudhibiti uwanja wa Tahrir, ikiwa ni sehemu muhimu ya waandamanaji kumtaka rais Hosni Mubarak aachie madaraka, wakilala katika mahema ama katika mablanketi chini ya vifaru vya jeshi.

Bango kubwa ambalo limeandikwa maandishi yasemayo, Umma unataka kuona mwisho wa utawala huu, limewekwa katika uwanja wa Tahrir, lakini kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 ameendelea kubaki madarakani bila kujali, akifanya tu mabadiliko ya baraza lake la mawaziri na kutoa ahadi za kufanya mageuzi lakini amekataa kung'atuka.

Muandamanaji mmoja mwenye umri wa miaka 60 amesema, na hapa namnukuu, " Tulikuwa waoga. tulikaa kimya miaka yote hii, lakini nyie mmeweza. Ni kitu kinachotia moyo. Ni kama kuzaliwa upya." mwisho wa kumnukuu.

Jana Mubarak amejaribu kuvuta wakati akiwa madarakani , kwa kuahidi kupandisha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta ya umma kwa asilimia 15 na kuamuru uchunguzi huru kuhusiana na ghasia zilizosababisha umwagikaji wa damu ambapo watu 300 wameuwawa katika muda wa siku 15 za maandamano. Ongezeko hilo la mshahara huenda likawahakikishia wafanyakazi wa serikali na majeshi ya usalama maslahi yao, lakini hakuna ishara kwamba waandamanaji wako tayari kuacha maandamano yao.

Siku ya pili ya mazungumzo baina ya serikali na makundi ya upinzani yanatarajiwa kufanyika tena leo Jumanne.

Wakati huo huo utawala wa rais Barack Obama unawahimiza viongozi wa Misri kuwajumuisha watu wengi zaidi katika mazungumzo hayo ya kitaifa kuhusu mageuzi, lakini haukutaka kuidhinisha madai ya waandamanaji wanaotaka rais Hosni Mubarak aondoke madarakani haraka iwezekanavyo.

Guido Westerwelle Pressekonferenz Ägypten
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: AP

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema uamuzi wa nani aiongoze Misri uko mikononi mwa umma wa nchi hiyo.

Wakati Marekani inasubiri kwa shauku maendeleo ya kisiasa katika nchi hiyo ambayo ni mshirika wake mkubwa miongoni mwa mataifa ya Kiarabu, maafisa wa utawala huo wanaonya kuwa kuondoka haraka kwa Mubarak kunaweza kurejesha nyuma hatua za mpito za kidemokrasia nchini humo.

Mwandishi : Sekione Kitojo / ape/ afpe/dpae

Mhariri :