1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mueller akamilisha uchunguzi wa Urusi na Trump

Bruce Amani
23 Machi 2019

Mwanasheria maalum nchini Marekani Robert Mueller amewasilisha ripoti yake ya siri kuhusu uchunguzi wa jukumu la Urusi katika uchaguzi wa rais wa 2016

https://p.dw.com/p/3FYCC
Portrait: Robert Mueller
Picha: picture-alliance/AP/C. Dharapak

Baada ya uchunguzi wa karibu miaka miwili ambao uliwanasa washirika wa zamani wa Trump na maafisa wa ujasusi wa Urusi na kuibua maswali kuhusu nafasi ya Trump katika wadhifa wa rais, Mueller aliikabidhi ripoti hiyo kwa Mwanasheria Mkuu William Barr.

Katika uchunguzi wake, Mueller aliwashitaki watu 34 na kampuni tatu. Swali sasa ni kama ripoti hiyo ina madai kuwa Trump alifanya makosa yoyote au kama inamuondolea lawama. Miongoni mwa watu hao ni aliyekuwa kiongozi wa kampeni za raos Paul Manafort na mshauri wake wa kwanza wa usalama wa taifa Michael Flynn. Warusi 25 walishitakiwa kwa mashitaka yanayohusiana na uingiliaji uchaguzi wakituhumiwa kwa ama kudukua akaunti za barua pepe za chama cha Democratic wakati wa kampeni au kupanga kampeni ya mitandao ya kijamii ambayo ilisambaza habari za uwongo kwenye intaneti. Wasaidizi watano wa Trump walikiri kuwa na hatia na wakakubaliana kushirikiana na Mueller katika uchunguzi wake.

USA William Barr
Barr anastahli kuwasilisha ripoti bungeniPicha: Getty Images/M. Wilson

Trump alikanusha madai kuwa alishirikiana na Urusi wakati wa kampeni za urais kwa ajili ya kupata ushindi. Urusi pia inakanusha kuingilia kwa njia yoyote uchaguzi huo

Sasa hatua inayofuata ipo mikononi mwa Barr, ambaye ana jukumu la kuandika ripoti yake kuhusu matokeo ya uchunguzi wa Mueller na kuituma katika Bunge la Marekani. Katika barua kwa wabunge, alitangaza kuwa amejitolea kuhakikisha uwazi na kuharakisha mchakato huo. Ikulu ya White House imejitenga na ripoti hiyo ikisema haijaiona wala kufahamishwa chochote kuihusu. Trump amesalia kimya kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Kuwasilishwa kwa ripoti hiyo ya Mueller kuna maana kuwa uchunguzi umekamilika bila mashitaka yoyote ya umma ya njama ya uhalifu kati ya timu ya kampeni ya Trump na Urusi au kizuizi kilichowekwa na rais huyo. Afisa wa Wizara ya sheria ya Marekani amethibitisha kuwa Mueller hatopendekeza mashitaka mengine zaidi.

Hizo ni habari nzuri kwa washirika kadhaa wa Trump na jamaa zake waliokumbwa na uvumi wa kuwa walifanya makosa. Ni pamoja na Donald Trump Jr., ambaye alikuwa na jukumu la kupanga mkutano na wakili aliyekuwa na mahusiano na serikali ya Urusi, kwenye jengo la Trump Tower wakati wa kampeni za urais 2016. Mwengine ni shemeji wa Trump, Jared Kushner, ambaye alihojiwa alau mara mbili na waendesha mashitaka wa Mueller.