1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mukwege akosoa matayarisho uchaguzi DRC

Mohammed Khelef
28 Agosti 2023

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kutokea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Dk. Denis Mukwege, amekosowa matayarisho ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaofanyika mwezi Disemba akisema yaanaashiria udanganyifu mkubwa.

https://p.dw.com/p/4Veu1
DR Kongo | Treffen Präsident Félix Tshisekedi & Denis Mukwege, Friedensnobelpreisträger
Picha: Giscard Kusema/Präsidentschaft der Demokratischen Republik Kongo

Mshindi huyo wa Tuzo ya Nobel mwaka 2018 aliwaambia vijana waliokusanyika kumsikiliza mbele ya jengo la Wakfu wa Panzi kwamba muundo wa sasa wa uchaguzi unaashiria udanganyifu mkubwa na wizi wa kura wakati wa kufanyika uchaguzi.

Mukwege, ambaye hadi sasa hajasema iwapo atagombea urais au la, alisema hayo jioni ya Jumapili (Agosti 27) akiwa mjini Bukavu, mkoa wa Kivu ya Kusini.

Soma zaidi: Mukwege awahimiza Wakongomani kuzuia wizi wa kura

Mbele ya mamia ya vijana hao, Mukwege aliukosoa utawala wa sasa chini ya Rais Felix Tshisekedi akisema "unaandaa uchaguzi ijapokuwa baadhi ya kadi za wapigakura tayari zimefutika na muda mfupi tu baada ya kumalizika kwa muda wa kuorodhesha wapigakura."

"Tunapokuwa na dosari za aina hii na hatuwezi kukasirika kusema kwamba njia inayoturuhusu kufanya uchaguzi wetu tayari imeharibiwa, tunaweza kutumaini nini tena?" Aliuliza Dk. Mukwege.

Wito wa maandamano ya umma

Kwa daktari huyo wa binaadamu, kufutika kwa kadi za uchaguzi ni ishara mbaya kwa wapigakura.

DR Kongo | Treffen Präsident Félix Tshisekedi & Denis Mukwege, Friedensnobelpreisträger
Rais Félix Tshisekedi anatuhumiwa na wakosoaji wake kwa kutaka kuuharibu uchaguzi wa Disemba 2023 kwa manufaa yake.Picha: Giscard Kusema/Präsidentschaft der Demokratischen Republik Kongo

Aliwataka raia ambao wamepatwa na mkasa huo kuandamana na kudai serikali iwajibike kwa kuwapa kadi mbovu za wapiga kura.

Soma zaidi: Upinzani wakosoa zoezi la usajili wa wapigakura nchini Congo

"Lakini tukinyamaza, tukaenda kwenye chaguzi ambazo zilishatayarishwa kuchakachuliwa, lazima niwaambie raia wa Kongo waisome historia ya nchi yao, wataona kuwa tangu zamani Wakongo hawajawahi kuongozwa na watu wa chaguo lao." Aliongeza. 

Mukwege alitoa wito kwa raia wa Kongo kutoka katika alichokiita "usingizi" na kuwa wazalendo halisi kwa ajili ya kuijenga upya nchi yao, akiamini kuwa wakongo kubaki kimya mbele ya maovu wanayotendewa ni usaliti.

Chama tawala cha UDPS kimetupilia mbali ukosoaji wa mshindi huyo wa Tuzo ya Nobel kikisisitiza kwamba uchaguzi unaandaliwa inavyostahili. 

Imetayarishwa na Mitima Delachance/DW Bukavu