1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mursi kukutana na Angela Merkel

Elizabeth Shoo30 Januari 2013

Rais Mohammed Mursi wa Misri leo anatarajiwa nchini Ujerumani ambapo atakutana na Kansela Angela Merkel mjini Berlin. Safari ya Mursi inakuja wakati ambapo hali nchini mwake sio shwari.

https://p.dw.com/p/17Tx5
Egyptian President Mohamed Mursi talks with U.S. Senator John McCain (not seen) during their meeting in Cairo January 16, 2013. REUTERS/Asmaa Waguih (EGYPT - Tags: POLITICS)
Mohammed MursiPicha: Reuters

Rais Mohammed Mursi alikuwa amepanga kufanya ziara ya siku mbili hapa Ujerumani na kisha kuelekea Ufaransa siku ya Ijumaa. Lakini sasa safari ya Ufaransa imefutwa na muda wa ziara ya Ujerumani kupunguzwa. Inatarajiwa kwamba Mursi atakuwepo Berlin kwa muda wa masaa machache tu. Mursi amepangiwa kukutana na Kansela Angela Merkel na vile vile atafanya mazungumzo na wawakilishi mbali mbali kutoka sekta ya biashara kwani nchi yake inakumbwa na mgogoro wa kiuchumi. Lengo la Mursi ni kutafuta wawekezaji watakaosaidia kuokoa uchumi wa nchi yake.

Akizungumza katika kituo cha televisheni cha ARD cha hapa Ujerumani, waziri wa mambo ya nje wa nchi hii Guido Westerwelle, amezitaka nchi nyingine ziwe na subira juu ya suala la Misri: "Misri ni mshirika wetu muhimu na ni nchi iliyowezesha mapinduzi katika ulimwengu wa Kiarabu kutokea. Ninashauri tuonyeshe uvumilivu kwa Misri. Tuseme tunachotaka kukosoa lakini tusiache kufanya mazungumzo. Mazungumzo ni njia bora zaidi ya ushawishi."

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: picture-alliance/dpa

Westerwelle amesema kuwa Ujerumani itatoa msaada kwa Misri iwapo tu nchi hiyo itafuata masharti fulani. Msaada utategemea kama patakuwa na maendeleo ya kidemokrasia. Westerwelle ameitaka serikali ya Misri kukaa pamoja na wapinzani na kufanya mazungumzo.

Hali ya uchumi bado ni tete

Safari ya Mursi inakuja wakati ambapo maandamano dhidi yake bado yanaendelea Misri. Watu 52 walipoteza maisha yao katika vurugu zilizotokea wakati wa maadhimisho ya miaka miwili baada ya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Hosni Mubarak.

Maandamano ya kumpinga Mursi katika mji mkuu wa Misri, Cairo
Maandamano ya kumpinga Mursi katika mji mkuu wa Misri, CairoPicha: Getty Images

Tatizo kubwa linaloikabili Misri kwa sasa ni la kiuchumi. Idadi ya watalii imepungua kwa kiasi kikubwa baada ya mapinduzi kutokea mwaka 2011. Hivi sasa Misri inahitaji wawekezaji kutoka nje. Hapa Ujerumani, wafanyabiashara wanaelewa kwamba Misri ni mahala pazuri pa kuwekeza lakini wanahofia hali ya usalama.

Mtaalamu kutoka taasisi ya biashara na viwanda Ujerumani, Steffen Behm, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba makampuni ya Ujerumani yanangojea kwanza hali ya kisiasa itulie kabla ya kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha nchini Misri.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayemaliza muda wake, Bi Hillary Clinton, amesema kuwa kuvunjika kwa uchumi wa Misri kutakuwa na athari kubwa katika maeneo mengi.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters

Mhariri: Saumu Yusuf