1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni amlaumu Kony

21 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CeOc

KAMPALA.Rais Yoweri Museveni wa Uganda amemshutumu kiongozi wa waasi wa LRA Joseph Kony kuwa hayuko tayari kwa mazungumzo ya amani, akigusia taarifa ya kwamba amemuua msaidizi wake Vicent Otti.

Kauli hiyo ya Rais Museveni inakuja baada ya taarifa kadhaa ya kwamba Joseph Kony amemuua msaidizi wake Otti ambaye alikuwa kiungo muhimu cha kuanza kwa mazungumzo ya amani mwaka 2005.

Rais Museveni amesema kuwa Kony amemuua Otii akimtuhumu kuwa alikuwa jasusi wa serikali, kitu kinachoashiria kuwa hataki amani.

Amesema kuwa pamoja na kwamba Vicent Otti alikuwa na makosa yake lakini alifanya juhudi kubwa za kuwepo kwa mazungumzo ya amani ikiwa ni pamoja na kumshawishi Joseph Kony kukutana na mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa Rais wa zamani wa Msumbiji Joachim Chissano.

Kundi la waasi la LRA katika miezi ya hivi karibuni limepata mapigo ikiwa ni pamoja na kujisalimisha kwa makamanda wake wa ngazi ya juu na kutojulikana kwa majaaliwa ya Vicent Otti na kutoa matumaini ya kumalizika kwa mzozo huo wa miongo miwili.