1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni kuwachukulia hatua wanajeshi wa Rwanda

7 Agosti 2020

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ametoa amri kwamba wanajeshi wa Rwanda wanaodaiwa kuingia nchini mwake na kuwateka nyara raia wachukuliwe hatua.

https://p.dw.com/p/3gdFg
Yoweri Museveni
Picha: picture-alliance/dpa/A. Novoderezhkin

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ametoa amri kwamba wanajeshi wa Rwanda wanaodaiwa kuingia nchini mwake na kuwateka nyara raia wachukuliwe hatua.

Agizo hilo limetolewa kwa wakuu wa wilaya zinazopakana na Rwanda kufuatia visa kadhaa vya raia wa Uganda kukamatwa na majeshi ya Rwanda wakiwa ndani ya mipaka ya Uganda.

Aidha, Rais amewataka raia wa Uganda kutothubutu kuvuka mpaka kwenda Rwanda, akisema wanaweza kushukiwa kushiriki biashara za magendo.

Kulingana na taarifa za ofisi ya rais Uganda, utawala wa Rwanda umeamrisha watu wanaopatikana wakishiriki biashara ya magendo kwenye mipaka na Uganda wapigwe risasi.

Hivi majuzi, maiti ya raia wa Uganda aliyedaiwa kutekwa nyara ilikabidhiwa kwa viongozi wa wilaya na wakuu wa serikali ya Rwanda.

Maagizo mapya ya Rais Museveni yanazusha mashaka kuhusu ufanisi wa juhudi za upatanishi kati ya Rwanda na Uganda, unaozihusisha Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.