1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa Muqtada al- Sadr wachukua uongozi wa mapema Iraq

Mohammed Abdulrahman
14 Mei 2018

Ushirika wa kisiasa wa imam wa Kishia mwenye ushawishi mkubwa nchini Iraq Muqtada al- Sadr, umechukuwa uongozi wa mapema katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/2xfzA
Irak, Bagdad: Portrait Muqtada al-Sad
Picha: picture-alliance/K. Kadim

Ushirika wa kisiasa wa imam wa Kishia mwenye ushawishi mkubwa nchini Iraq Muqtada al- Sadr, umechukuwa uongozi wa mapema katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, ikiwa ni kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliotangazwa na Tume ya uchaguzi ya nchi hiyo. 

Matokeo hayo yalianza kujulikana saa 24 baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa kote nchini , kukiwa na  ushiriki mdogo. Matokeo hayo ni pamoja na  yale kamili kutoka mikoa 10 kati ya 19, ikiwemo Baghdad na Basra. Waziri mkuu  Haider al-Abadi anasemekana amepata matokeo mabaya katika mikoa yenye wakaazi wengi wa Kishia. Ushirika wa wagombea wenye mafungamano na makundi ya wanamgambo wa Kishia ulikuwa nafasi ya pili. Hadi tume inamaliza kutangaza matokeo ya awali, orodha ya wagombea wa al-Sadr ilikuwa na kura nyingi zaidi. Tume ya uchaguzi imesema ni 44 asilimia ya wenye haki ya kupiga kura ndiyo walioshiriki katika uchaguzi huo.

Shangwe iliibuka mjini Baghdad, hasa katika eneo  la wakaazi masikini  kiasi ya milioni 3 na ambalo limepewa jina la baba yake Sadr, marehemu Ayatollah Mohammad Sadq al-Sadr. Sadr mdogo aliongoza kampeni ya uchaguzi akiahidi kupambana na rushwa na ufisadi  serikalini na  kuwekeza zaidi  katika masuala ya jamii, kuboresha huduma kwa umma, huku akiunda ushirika uliowashangaza wengi na chama  cha Kikoministi katika mji mkuu.

Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi
Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-AbadiPicha: picture-alliance/dpa/AP

Waziri mkuu Al-Abadi ambaye  akiwania kuendelea  kuwa waziri mkuu baada ya kulisimamia jeshi katika mapambano dhidi ya wapiganaji wa  kundi la  Dola la Kiislamu IS, amekabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa mtangulizi wake Nouri-al maliki pamoja na  Sadr na wagombea wa ushirika wa Fatah, ambapo  makamanda wa wanamgambo hao walilazimika kujiuzulu ili kuweza kuwa wagombea.

Matokeo mazuri upande wa fatah yanaonekana kama ni ushindi  kwa Iran, ambayo inapigania kulinda masilahi yake, pamoja na wanamgabo inaowafadhili kifedha ambapo baadhi ya wakati imewaamuru kupigana bega kwa bega na wanajeshi wake nchini Syria. Al-Sadr ni hasimu mkubwa  wa ushawishi wa Iran na marekani katika siasa za Iraq.

Uchaguzi mkuu wa Jumamosi ulikuwa wa kwanza  tangu Iraq ilipotangaza ushindi wa dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu na wa nne tangu uvamizi ulioongozwa na  Marekani 2003, kumuangusha madarakani Saddam Hussein. Chama  cha kisiasa au  Ushirika unalazimika kupata wingi wa viti 329 bungeni kuweza kumchagua Waziri mkuu na kuunda serikali . Panatarajiwa mazungumzo kati ya pande mbali mbali kuweza  kupata viti 165 vinavyohitajika. hadi wakati huo, Waziri mkuu al-Abadi atabkia madarakani akiwa na madaraka kamili. Katiba imetenga  orodha mahsusi kwa uawakilishi wa wanawake. Karibu wanawake 2,600 wanagombea ubunge safari hii.

Mwandishi : Mohammed Abdul-Rahman, ap

Mhariri: Iddi Ssessanga