1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka mmoja tangu kuachiwa mripuaji wa ndege huko Lockerbie

Kabogo Grace Patricia18 Agosti 2010

Mripuaji huyo Abdel Baset al-Megrahi aliachiwa huru kutoka jela mwaka uliopita kwa kuzingatia misingi ya huruma kutokana na kuugua saratani ya kibofu.

https://p.dw.com/p/OqK7
Abdel Baset al-Megrahi (Kati) akisaidiwa kushuka kwenye ndege baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Tripoli, Libya.Picha: AP

Ikiwa ni mwaka mmoja sasa tangu mripuaji wa ndege ya Pan Am katika eneo la Lockerbie, Scotland, Abdel Baset al-Megrahi, aachiwe huru kutoka jela moja ya Scotland kwa misingi ya huruma kutokana na kuugua saratani, viongozi nchini Uingereza wako katika shinikizo la kuwataka wafafanuwe kwa kina sababu zilizoifanya serikali iliyopita ya chama cha Labour kuchukua uamuzi huo.

Abdel Basset al-Megrahi, raia wa Libya, aliyeachiwa na viongozi wa Scotland Agosti 20, mwaka uliopita kutokana na kuugua saratani ya kibofu ambayo madaktari walisema alikua na miezi mitatu tu ya kuishi, bado yuko hai hadi sasa na anaishi na familia yake kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli ambako imeripotiwa anaendelea na matibabu. Mjadala umezuka baada ya mripuaji huyo wa ndege ya abiria ya Marekani ya Pan Am katika eneo la Lockerbie, mwaka 1988 na kuwaua watu 270, wakiwemo raia 189 wa Marekani kuendelea kuwa hai hadi sasa tofauti na ilivyoelezwa na madaktari. Lakini kwa upande mwingine baadhi ya wakosoaji wanaona kuwa mazingira ya kuachiwa al-Megrahi hayakuwa kwa sababu za ugonjwa peke yake.

Balozi wa zamani wa Uingereza nchini Libya, Richard Dalton ameliambia shirika la habari la Ujerumani-DPA, kuwa uamuzi wa kuachiwa mripuaji huyo ulizingatia misingi hiyo ya huruma, lakini pia ulikua uamuzi uliokuwa wa kuchukiza. Al-Megrahi, mwenye umri wa miaka 58 jasusi wa zamani wa Libya, siku zote amekuwa akikanusha kuhusika na uripuaji huo wa ndege. Mwaka 2001, alihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kesi yake kusikilizwa kwa muda mrefu, na hadi anaachiwa huru mwaka uliopita alikuwa ameshatumikia kifungo cha miaka minane jela. Baada ya kurejea Libya, al-Megrahi alipokelewa kishujaa na serikali ya nchi hiyo.

Hasira miongoni mwa ndugu za Wamarekani waliouawa katika shambulio hilo ziliibuka tena kutokana na uamuzi wa kuachiwa mripuaji huyo kuhusishwa na kampuni ya mafuta ya Uingereza ya BP. Aidha, maseneta wa Marekani wamezusha maswali mapya kuhusu uhusiano uliokuwepo kati ya BP na uamuzi wa kuachiwa huru al-Megrahi. Kampuni ya BP inadaiwa kuwa ilishawishi kuachiliwa kwa al-Megrahi ili kuweza kurahisisha mikataba ya mafuta na Libya. Nchini Scotland viongozi wako katika shinikizo la kuchapisha taarifa zote za ugonjwa wa al-Megrahi ambao Waziri wa Sheria wa Scotland, Kenny MacAskill alizingatia katika uamuzi wa kuachiwa mripuaji huyo katika mazingira ya huruma.

Kuachiwa huru al-Megrahi kunahusishwa na mkataba wa dola milioni 900 wa kuchimba mafuta na gesi uliosaniwa kati ya Libya na kampuni ya BP mwaka 2007, mwaka ambao pia Uingereza na Libya zilisaini makubaliano ya kuhamishwa mfungwa. Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron ambaye alilaani vikali uamuzi huo wa Scotland, ametupilia mbali madai ya Marekani ya kutaka kufanyika uchunguzi mpya. Aidha, Balozi Dalton amesisitiza kuwa hakuna uhusiano wowote kati ya kuachiwa al-Megrahi na maslahi ya kibishara ya kampuni ya BP. Hata hivyo kumekuwa na taarifa kwamba mripuaji huyo anaweza akaishi kwa miaka mingine kumi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE)

Mhariri:M.Abdul-Rahman