1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpinzani Zimbabwe akutwa amekufa baada ya kutekwa nyara

14 Novemba 2023

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbwabwe kimesema mwanaharakati wake ,Tapfumaneyi Masaya amekutwa amekufa,baada ya kutekwa nyara Jumamosi wakati wa kampeini ya kisiasa nje ya mji mkuu Harare.

https://p.dw.com/p/4Yo86
Simbabwe Afrika Veranstaltung Opposition
Chama cha CCC kimesema mwanaharakati wake amekutwa amekufa baada ya kutekwa.Picha: KB MPOFU/REUTERS

Chama cha Citizens Coalition for Change, CCC kimesema mwanaharakati huyo aliingizwa kwenye gari na watu wasiojulikana wakati alipokuwa akishiriki shughuli ya kampeini ya mgombea wa chama hicho kabla ya uchaguzi ujao wa marudio utakaofanyika Desemba 9.

Msemaji wa chama hicho Promise Mkwananzi amesema mwanaharakati huyo aliiteswa na kisha kutupwa nje ya mji mkuu Harare.Hata hivyo shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha juu ya tukio hilo.

Soma pia: Chamisa alitaka bunge liwarudishe wabunge 15 wa chama chake

Kutekwa nyara na kuuwawa kwa Masaya kumetokea katika kipindi cha takriban wiki mbili baada ya tukio jingine, la kutekwa ,kuteswa,na kisha kutupwa,na watu waliokuwa na silaha, mwanasheria Takudzwa Ngadiore.

Zimbabwe ina historia ya muda mrefu ya matukio kama hayo ya kuuwawa kwa wanaharakati wa kisiasa na Upinzani mara nyingi umekuwa ukituhumu,yanafanywa na chama tawala cha Zanu PF.