1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kuwarejesha Warohingya nyumbani yatiwa saini

Amina Mjahid
6 Juni 2018

Makubaliano yamesainiwa baina ya serikali ya Myanmar na mashirika ya Umoja wa Mataifa, kuhusu kuanza kurejea nyumbani kwa wakimbizi wa Rohingya wapatao 700,000.

https://p.dw.com/p/2z22o
Bangladesch Rohingya-Flüchtlinge in Palong Khali
Picha: picture-alliance/dpa/B. Armangue

Mkataba wa maelewanao uliofikiwa unaahidi kuweka mpango wa ushirikiano unaonuia kujenga mazingira ya hiari, yalio salama, ya heshima na endelevu katika kuwahamisha wakimbizi wa Rohingya, lakini hauzungumzii kukataa kwa serikali ya Mnyanmar kuwapa uraia watu wa jamii hiyo ya wachache nchini humo.

Serikali ya Myanmar imesema inatumai mpango huo utaharakisha zoezi la kuwahamisha wakimbizi wa Rohingya. Hata hivyo makundi ya kutetea haki za binaadamu yanatilia shaka iwapo idadi kubwa ya wakimbizi hao watakubaliwa kurejea nyumbani au hata iwapo serikali hiyo ya Myanmar itatoa ulinzi wa kutosha kwa wale watakaorejea.

Bangladesch Myanmar - Grenzgebiet Rohingya - Flüchtlinge
Picha: Getty Images/AFP/T. Mustafa

Taarifa ya Myanmar haikutaja neno Rohingya hali inayoonyesha msisitizo kutoka katika serikali na raia wengi wa nchi hiyo, kwamba hakuna kabila kama hilo nchini Mnyanmar. Badala yake inawatambua kama watu waliyopoteza makaazi.

Aidha vikosi vya usalama vya Myanmar vimedaiwa kuhusika na visa vya ubakaji, mauaji, mateso na kuchoma nyumba za warohingya Magharibi mwa jimbo la Rakhine wanakoishi warohingya wengi. Umoja wa Mataifa pamoja na Marekani wameelezea hali ya ukandamizaji unaodaiwa kufanywa na jeshi kuanzia mwezi Agosti mwaka jana kama hatua ya kuitokomeza jamii hiyo.

Wakimbizi wa Rohingya wahofia maisha yao yapo hatarini nchini Myanmar

Kwa kiasi kikubwa Myanmar na Bangladesh walikubaliana mwezi Novemba kuanza kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Rohingya. Lakini wakimbizi hao wanahofia kuwa maisha yao huenda yakawa hatarini nchini Mnyanmar bila ya uangalizi wa kimataifa. Myanmar inasisitiza ina hati za utambulisho ambazo zimekataliwa na warohingya wengi.

Knut Ostby, Mratibu wa masuala ya kiutu katika shirika la Umoja wa Mataifa na ni mkaazi nchini Mnyamar anasema makubaliano yaliyofikiwa ni hatua moja muhimu ya kutatua mgogoro uliopo.

Rehana Khatun RohingyRohingya Frau mit Kind
Picha: Reuters/M. Ponir Hossain

"Tunazungumzia wakimbizi takriban 700,000 ambao sio tu wanapaswa kurejea nyumbani lakini pia mazingira yanapaswa kuwa sawa kwa wao kurejea, namaanisha usalama wao, utambulisho wao, huduma, mahali pa kuishi na miundombinu," alisema Knut Ostby.

Kwa upande wake Umoja wa Mataofa umesema makubaliano hayo yanafungua njia ya mashirika yake yanayoshughulikia wakimbizi na mashirika ya maendeleo kupewa nafasi ya kufikia jimbo la Rakhine. Takriban warohingya 125,000 waliobakia nchini Myanmar wanaishi katika makambi ambako mienendo yao inadhibitiwa baada ya kulazimika kuondoka vijijini mwao mwaka 2012 kufuatia vurugu zilizoongozwa na wa wafuasi wa madhehebu ya Boudha na vikosi vya usalama.

"Bado hakuna mienendo yoyote inayoonyesha warohingya wana haki sawa ya kupata uraia'', alisema Matthew Smith, mkuu wa makundi ya kutetea haki za binaadamu. Smith anasema hatua ya kuwahamisha wakimbizi kwa sasa inaonekana kuwa jaribio la serikali ya Myanmar kufunika  mateso makubwa na uhalifu ulioendelea.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AP

Mhariri: Gakuba, Daniel