1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar yahimizwa kuchunguza ghasia za kidini

MjahidA1 Aprili 2013

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limeihimiza Myanmar kuchunguza ni kwanini maafisa wa polisi wameshindwa kusimamisha wimbi la mauaji kati ya Waislamu na waumini wa dini ya Budha.

https://p.dw.com/p/187nC
Picha za satalaiti za Human Rights watch
Picha za satalaiti za Human Rights watchPicha: Human Rights Watch/Astrium/DigitalGlobe/EUSI

Human Rights Watch imetoa picha za satalaiti zinazoonesha majengo takriban 800 yakiwa yameharibiwa kabisa katika mji wa Meiktila. Mkurugenzi wa shirika hilo katika eneo la Asia, Brad Adams, amesema serikali inapaswa kuchunguza sababu halisi ya ghasia za Meiktila na ni kwa nini polisi walishindwa kuzuia mauaji pamoja na kuharibiwa kwa majengo katika eneo hilo.

Kulingana na shirika la habari la Myanmar, ghasia za mwezi uliopita zilizosambaa hadi katika miji mingine zilisababisha mauaji ya watu 43 huku nyumba zaidi ya 1,300 na majengo mengine yakiharibiwa katika nchi hiyo iliyokuwa zamani ikiendeshwa na utawala wa kijeshi.

Vikosi vya jeshi Myanmar
Vikosi vya jeshi MyanmarPicha: AFP/Getty Images

Kwa upande wake Umoja wa Mataifa umesema takriban watu 12,000 wameachwa bila makaazi kutokana na ghasia hizo. Maeneo yalioathirika vibaya zaidi katika eneo la Meiktila ni vijiji ambavyo vilikuwa vinakaliwa na idadi kubwa ya Waislamu.

Umoja wa Mataifa umesema kuna habari nyingi walizopata ambazo zinaashiria kuwa polisi waliridhia mapigano hayo kati ya Waislamu na waumini wa Budha na ndio maana walikaa kando bila ya kuyaingilia.

Rais Thein Sein atoa onyo

Hata hivyo, kwa sasa hali ni shwari na hii ni baada ya Rais Thein Sein wa Myanmar kuapa kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale wanaosababisha ghasia hizo za kidini. Rais Sein amesema ghasia hizo zinaharibia sifa taifa hilo, linalojulikana pia kama Burma.

Rais wa Myanmar Thein Sein
Rais wa Myanmar Thein SeinPicha: JOHN THYS/AFP/Getty Images

Wakati huo huo, Rais Sein aliwataka wajumbe wa waumini Buddhah kuisaidia serikali kuendeleza amani na udhabiti wa nchi.

Shirika la Human Rights Watch limeitaka serikali kuacha ubaguzi na kuhimiza uwiano wa dini ili kumaliza mashambulizi dhidi ya Waislamu nchini humo. Shirika la Ushirikiano la Waislamu limesema litaandaa mkutano Aprili 14 nchini Saudi Arabia kuzungumzia hali halisi nchini Myanmar.

Magazeti ya kibinafsi kufanya tena kazi

Huku hayo yakijiri, mashirika manne ya kibinafsi ya habari yameanza tena kufanya kazi hii leo baada ya miaka 50 ya kufungiwa. Hii ni baada ya serikali ya Myanmar kutoa vibali kwa mashirika 16 ambayo manne pekee ndio yalioanza kazi hii leo.

Inasemekana hatua hiyo imechukuliwa ili kutoa ushindani kwa gazeti la kiongozi wa upinzani nchini humo Aung San Su Kyi pamoja na gazeti la D Wave yanayotayarishwa kwa uzinduzi.

Toleo la gazeti la kibinafsi
Toleo la gazeti la kibinafsiPicha: Reuters

Serikali iliyopigiwa kura iliingia madarakani mwaka wa 2011 baada ya takriban muongo mmoja wa kuongozwa na jeshi.

Serikali hiyo ilianza kufanya mabadiliko katika mfumo wa vyombo vya habari kama njia moja ya kuwa na demokrasia nchini humo.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef