1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar yawaachia waandishi wa Reuters

Lilian Mtono
7 Mei 2019

Waandishi wawili wa habari wa shirika la habari la Reuters waliokuwa kizuizini nchini Myanmar baada ya kuripoti kuhusu mzozo wa Rohingya wamechiliwa huru baada ya msamaha wa rais.

https://p.dw.com/p/3I3wR
Myanmar Journalisten
Picha: picture-alliance/AP Images/A. Wang

Wa Lone na Kyaw Soe Oo walilakiwam na waandishi wenzeo wa habari baada tu ya kutoka nje ya geti la gereza kuu la Yangon, baada ya kuwepo kizuizini kwa zaidi ya miezi 16. Waandishi hawa ni miongoni mwa wafungwa 6,000 walioachiwa chini ya msamaha huo wa rais.

Kukamatwa kwa waandishi hawa Disemba 2017, kuliibua taswira ya mbinyo wa uhuru wa habari katika taifa la Myanmar linaloongozwa na mshindi wa tuzo ya kimataifa ya amani ya Nobel Aung San Suu Kyi.

Wa Lone, 33, aliwashukuru watu kwa jitihada zao za kushinikiza kuachiwa kwao huru na kuapa kwamba atarejea kazini. "Nina hamu sana ya kurejea kwenye chumba cha habari" alisema "Mimi ni mwandishi wa habari na nitaendelea kuwa hivyo".

Mhariri mkuu wa Reuters Stephen Adler amesema "Tumefurahishwa sana na hatua ya Myanmar ya kuwaachilia huru waandishi wetu". "Tangu kukamatwa kwao siku 115 zilizopita, wamekuwa alama ya umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari kote duniani. Tunawakaribisha."

Myanmar, Yangon: Die Journalisten Kyaw Soe Oo und Wa Lone
Mwandishi Wa Lone akisindikizwa na polisi kwenda kortini, Julai 16,2018.Picha: Reuters/A. Wang

Msemaji wa serikali ya Myanmar Zaw Htay ameliambia shirika la habari la Reauters kwamba jamaa wa waandishi hao walituma barua kwa Suu Kyi na rais Win Myint. "Baada ya viongozi hao kuangazia maslahi ya muda mrefu ya taifa hilo, hatimaye waliamua kuwaachilia waandishi hao."

Umoja wa Mataifa umesifu hatua hiyo, lakini ikionya kwamba uhuru wa kujieleza nchini humo bado kwa kiasi kikubwa unabinywa. "Ni habari njema..., hali ya uhuru wa kujieleza (Myanmar) bado iko katika hali mbaya", alisema msemaji wa ofisi ya haki za binaadamu katika umoja huo Ravina Shamsadani kwa waandishi wa habari mjini Geneva.

Waandishi hao walihukumiwa kifungo cha miaka 7 gerezani kwa kukiuka sheria ya siri za serikali.

Waliripoti kuhusu mauaji ya jamii ya Waislamu 10 wa Rohingya yaliyofanyika Septemba 2017, katika jimbo lililokumbwa na mzozo la Rakhine. Kufuatia mzozo huo, watu hao wapatao 740,000 wasio na utaifa walilazimika kukimbilia kwenye mpaka wa Bangladesh.