1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Ghuba wafika mahakamani

Lilian Mtono
28 Juni 2018

Umoja wa Falme za Kiarabu umepinga madai yaliyotolewa na Qatar dhidi yake katika mahakama ya sheria ya kimataifa ya ICJ, na kuyataja madai hayo ya Qatar kuwa yasiyo na msingi wowote. 

https://p.dw.com/p/30UKc
Völkermord Serbien Kroatien Prozess Den Haag
Picha: picture-alliance/AP

Umoja wa Falme za Kiarabu umepinga madai yaliyotolewa na Qatar dhidi yake katika mahakama ya sheria ya kimataifa ya ICJ, kwamba vizuizi vya mwaka mzima ilivyowekewa na mataifa ya Kiarabu, vimehujumu haki za binadamu za raia wake, ikiyataja madai hayo ya Qatar kuwa yasiyo na msingi. 

Mwaka mmoja tangu mataifa manne ya Kiarabu yalipokata mashirikiano ya kidiplomasia na kiuchumi na Qatar, taifa hilo dogo la Ghuba linataka zuwio la muda dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu na kuitaka Mahakama hiyo ya sheria ya Kimataifa - ICJ kuamuru kuondolewa kwa vizuizi hivyo.

Saudi Arabia, Misri, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu ziliiwekea Qatar vizuizi vya anga na baharini mnamo mwaka uliopita, kwa tuhuma kwamba taifa hilo linaunga mkono na kufadhili ugaidi. Qatar inakana madai hayo. Umoja wa Falme za Kiarabu uliongoza hatua hiyo, na Qatar imetoa madai yake ikirejea mkataba wa Umoja wa Mataifa unaozuia ubaguzi kwa kuzingatia utaifa.

Mwanasheria wa Umoja wa Falme za Kiarabu, alipozungumza mbele ya mahakama, iliyoko mjini The Hague hii leo alirudia madai yao ya awali kama kithibitisho cha kizuizi, akisisitiza kwamba Qatar inaunga mkono ugaidi.

Bildergalerie Straßenverkehr
Qatar inadaiwa kuunga mkono ugaidi na hatimaye kutengwa na mataifa manne ya KiarabuPicha: picture-alliance/Anka Agency/E. Nathan

Umoja wa Falme za Kiarabu wapinga madai ya Qatar.

Mwakilishi wa Qatar hapo jana alidai kwamba raia wa taifa hilo walirejeshwa kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu, lakini pia walizuiwa kupata huduma za afya na uhuru wa kujieleza. Haijawa wazi ni lini mahakama hiyo itatoa uamuzi wa madai hayo ya Qatar.

Wakili wa Qatar Mohammed Al-Khulaifi hapo jana alisema mbele ya majaji wa ICJ kwamba kwa miongo mingi Waqatar na Emirati walifanya kazi pamoja, walisali pamoja na hata kuoana miongoni mwa familia zao. Amesema licha ya mahusiano hayo ya karibu, Umoja wa falme za Kiarabu bado ulichukua hatua za kibaguzi dhidi ya taifa hilo na watu wake.

Lakini wakili wa UAE amemkosoa mwenzake wa Qatar alipokuwa akijibu hoja zake hii leo. Tullio Treves amesema picha iliyotengenezwa na Qatar kwenye madai yake kwamba raia wa Qatar waliondolewa UAE bila ya kosa pamoja na zuio la raia hao kuingia nchini humo ni upotoshaji mkubwa.

Amesema mahakama inatakiwa kuikataa kesi hiyo kwa kuwa Qatar haikutumia njia yoyote mbadala ya kusuluhisha madai ya ukiukwaji wa mkataba huo, ikiwa ni pamoja na njia ya diplomasia. Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar kwa pamoja walitia saini mkataba wa kimataifa wa kuondoa aina zote za ubaguzi wa rangi, unaojulikana, CERD, ambao unazuia ubaguzi kwa misingi ya utaifa. Saudi Arabia, Bahrain na Misri hawakusaini mkataba huo.

Balozi wa UAE nchini Uholanzi Saeed Alnowais ameiambia mahakama hiyo kwamba mara kadhaa serikali yake imeiomba Qatar kuachana na mwenendo wake, lakini Qatar ilirudia makosa yake mara kwa mara. Imeshindwa kusimamia wajibu wake, alisisitiza balozi huyo. Mapema mwezi huu Qatar iliishitaki Emirati katika mahakama hiyo inayohusika na usuluhishi wa mizozo kati ya nchi na nchi, ikiituhumu kwa ubaguzi wa rangi na ukiukwaji wa haki za binaadamu dhidi ya raia wake.

Mwandishi: Lilian Mtono/rtre/dpae/afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga