1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa kibiashara watishia kughubika mkutano wa G7

Caro Robi
8 Juni 2018

Nchi za Umoja wa Ulaya na Canada, mwenyeji wa mkutano wa kilele wa nchi saba zilizostawi kiviwanda G7 zimemuonya Rais wa Marekani Donald Trump kuwa hawatatishwa naye licha ya wasiwasi wa kuzuka vita vya kibishara.

https://p.dw.com/p/2z85Q
G7 Gipfel in Kanada
Picha: Reuters/B. Nelms

Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau amemuonya Trump kuwa hawatatetereka kuhusiana na nyongeza ya kodi juu ya bidhaa za chuma na bati. Na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema atakutana na viongozi wa Uingereza, Ujerumani na Italia kufikia msimamo wa pamoja kabla ya kukutana na Trump katika mkutano huo wa G7 unaoanza leo.

Kupitia ukurasa wa Twitter, Macron amesema rais wa Marekani huenda asijali kutengwa na washirika, lakini pia nao hawatajali kutia saini makubaliano ya kibiashara yanayohusisha nchi sita iwapo kutakuwa na haja ya kufanya hivyo.

Macron na Trump warushiana maneno

Akitumia lugha ya Kiingereza, Macron amesema nchi hizo sita zinawakilisha misingi ya maadili, soko la kiuchumi ambalo lina uzito kihistoria na ambazo ndizo dola halisi zenye nguvu zaidi kimataifa.

G7 Treffen Sizilien Donald Trump, Shinzo Abe, Justin Trudeau, Jean-Claude Junker, Angela Merkel, Emmanuel Macron
Baadhi ya viongozi wa G7 akiwemo Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Trump amewajibu Trudeau na Macron kupitia ukurasa wa Twitter kwa kuwaambia kuwa wanazitoza bidhaa za Marekani kodi ya juu na kuweka vizingiti dhidi ya biashara za nchi yake.

Trump ambaye alikutana na Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe hapo jana mjini Washingtion, huenda kwa hivi sasa mawazo yake yote yako katika mkutano ujao wa kilele kati yake na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un utakaofanyika Jumanne wiki ijayo, lakini ameweka wazi kuwa hana nia ya kulegeza kamba kuhusiana na suala la nyongeza ya kodi.

Mvutano kati ya Marekani na washirika wake ni mkubwa kiasi cha baadhi ya wachambuzi kupendekeza kuwa mkutano wa kilele wa G7 ubadilishwe jina na kuitwa G6 na Moja, huku Macron akisema viongozi wa nchi sita zinazounda G7 hawapaswi kusita kufikia makubaliano bila ya Trump.

Je, G7 itasambaratika?

Mvutano huo unatishia kulitikisa kundi hio ambalo kwa miaka 43 iliyopita limekuwa likijaribu kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu masuala ya kibiashara na mengineyo.

Kanada Whistler Treffen der G7 Finanzminister
Mawaziri wa fedha wa nchi wanachama wa G7Picha: picture-alliance/The Canadian Press/J. Hayward

Lakini wachambuzi wanasema kundi hilo la nchi zilizostawi zaidi kiviwanda duniani halijawahi kukosa kuafikiana kuhusu kauli yao ya mwisho katika mikutano ya kilele hata mwaka 1985 ambapo nchi hizo zilikuwa zimegawanyika kutokana na mzozo wa kibiashara.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel tayari amekiri kuwa itakuwa vigumu kwa nchi hizo za G7 zinazokutana kwa siku mbili kaskazini mwa mji wa Quebec, kukubaliana kuhusu masuala kadhaa ikiwemo hata taarifa ya mwisho ya pamoja.

Tangu kuingia madarakani mwezi Januari mwaka uliopita, Trump ameiondoa Marekani kutoka makubaliano kadhaa ya kimataifa ikiwemo makubaliano ya mazingira ya Paris, yale yanayohusu mpango wa kinyuklia wa Iran na wa biashara huru kati ya nchi za ukanda wa Pasifiki yanayojulikana kama TPP.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga