1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Mashariki:Syria kuwa mshirika mpya wa karibu

Thelma Mwadzaya17 Septemba 2010

Marekani ina mpango wa kuzishirikisha Syria na Lebanon kuzungumza pamoja na Israel kama hatua muhimu ya kuisaka amani ya kudumu ya Mashariki ya Kati kama ilivyoelezwa kwenye makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2002.

https://p.dw.com/p/PEG4
Viongozi wa Mashariki ya Kati walipoanza mazungumzo ya ana kwa anaPicha: AP

Kulingana na hati hiyo iliyozinduliwa kwenye kikao cha kilele cha mataifa ya Kiarabu mjini Beirut,Israel itatambuliwa na mataifa yote ya Kiarabu endapo itaondoka kwenye maeneo iliyoyateka nyara mwaka 1967 wakati wa vita vya Mashariki ya Kati ikiwemo Jerusalem Mashariki.

Kauli hizo zimetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton akiwa mjini Amman, baada ya kukutana na Mfalme Abdulla wa Pili wa Jordan.Kwa mujibu wa Bibi Clinton,viongozi hao wamejitolea na wana nia ya kuyatafutia suluhu mambo mazito yanayowakabili.

Akizungumza na waandishi wa habari na mwenzake wa Jordan Nasser Judeh,Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton alisema anaamini kuwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas,wanaweza kufanikiwa kutafuta suluhu ya mzozo huo.

Arabische Außenminister in Amman Jordanien
Kikao cha Umoja wa Mataifa ya Kiarabu cha Jordan na mwenyeji wake Mfalme Abdallah wa Pili:Makubaliano ya 2002 yalifikiwa kwenye kikao kama hikiPicha: AP

Hata hivyo, majadiliano hayo ya ana kwa ana kati ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na Rais wa Wapalestina, Mahmoud Abbas, yaliyoanzishwa upya hivi karibuni yanakabiliwa na hatari ya kuvunjika. Tatizo ni ujenzi wa makaazi ya Wayahudi ikiwa ujenzi huo utaanzishwa upya baada ya kusitishwa kwa miezi 10. Muda huo unamalizika mwisho wa mwezi huu wa Septemba.

Rais wa Misri, Hosni Mubarak, katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Israel, amesema kuwa alipokutana na Netanyahu siku ya Jumatano alitoa pendekezo la kurefusha muda huo kwa miezi mitatu mingine huku majadiliano ya amani yakiendelea. Wakati huo huo, unaweza kutumiwa kujadili suala la mipaka ya taifa la Palestina. Amesema makubaliano yakipatikana kuhusu mipaka hiyo, Israel itaweza kujenga ndani ya mipaka hiyo mipya sawa na Wapalestina pia. Kwa njia hiyo watatenzua tatizo la kurefusha upya muda wa ujenzi wa makaazi ya walowezi na wakati huo ukatumiwa kuendelea na majadiliano ya amani.

Israel kwa upande wake imesema kuwa makubaliano kama hayo yangeweza kuzingatia mpango wa kubadilishana ardhi, ambao utairuhusu Israel kubakia na sehemu kubwa ya makaazi ya Wayahudi katika Ukingo wa Magharibi.

Israel Palästina Palästinenser Siedlung Siedlungsbau Jerusalem Ramat Sholmo Ostjerusalem Flash-Galerie
Mtaa wa Ramat Sholmo,Jerusalem Mashariki:Mzozo wa fitna Mashariki ya KatiPicha: AP

Wakati huo huo, duru zilizo karibu na majadiliano hayo ya amani zimesema Marekani ilitoa pendekezo kama hilo na limekataliwa na Netanyahu ambae serikali yake ya muungano inadhibitiwa na vyama vinavyotaka kuendelea kujenga makaazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi. Lakini taarifa iliyotolewa na ofisi ya Netanyahu imesema haitotamka cho chote kuhusu yale yanayojadiliwa. Hata hivyo, msimamo wa Netanyahu uko pale pale, yaani hatorefusha muda wa kusitisha ujenzi wa makaazi hayo - lakini anadhamiria kudhibiti kiwango cha ujenzi huo katika siku zijazo.

Serikali ya Hamas inayodhibiti Ukanda wa Gaza imepinga uamuzi wa Rais Abbas kurejea katika majadiliano  yanayosimamiwa na Marekani. Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Amr Moussa, amesema majadiliano hayo ya amani yanafanywa katika kile kilichoitwa " hali ya shaka - shaka na wasiwasi." Mawaziri wa nje wa nchi za Kiarabu wanaokutana mjini Cairo wamesema wataendelea kuinyoshea Israel mkono wa amani. Wakati huo huo wametoa mwito kwa Wapalestina kumaliza tofauti zao za maoni ili kuimarisha msimamo wao katika majadiliano yanayoendelea.