1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa uhamiaji waitikisa serikali ya Merkel

Sekione Kitojo
19 Juni 2018

Washirika wa kansela Angela Merkel wa kihafidhina kutoka jimbo la Bavaria nchini Ujerumani wamekubali kumpatia muda wa wiki mbili wa  kupumua, ili apate suluhisho katika Umoja wa Ulaya kuhusiana na mvutano wa uhamiaji. 

https://p.dw.com/p/2zpZq
Horst Seehofer und Kanzlerin Merkel
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Hali  hiyo inatishia kuiporomosha serikali  ya  muungano  inayoongozwa  na  kansela  Merkel  ambayo  imedumu kwa  muda  wa miezi mitatu  hadi  sasa.

Kanada G7 Gipfel in Charlevoix Macron und Merkel
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kushoto) na kansela Angela Merkel wa Ujerumani (kulia)Picha: picture-alliance/empics/J. Tang

Wakati  huo  huo Merkel  na rais  wa  Ufaransa  Emmanuel Macron wanapambana  kuweza kupata  msimamo  wa  pamoja  katika  mageuzi  ya  Umoja  huo kabla  ya  mkutano  muhimu  mwishoni  mwa  mwezi  huu ambao unaweza  kuelekeza  hatima  ya  kundi  hilo  mla  mataifa.

Chama  cha  jimbo  la  Bavaria  cha  Christian Social Union , CSU, kina  wasiwasi  wa  kupoteza  wapiga kura kwa  chama  kipya  cha siasa  kali  za  mrengo  wa  kulia  katika  uchaguzi  wa  jimbo  mwezi Oktoba, na  kinataka  pachukuliwe  hatua  ya  kupiga  marufuku wahamiaji  kuingia  nchini  Ujerumani kwa wale  waliokwisha andikishwa   katika  nchi  nyingine  ya  Umoja  wa  Ulaya.

Rais  wa  Marekani  Donald Trump, akitetea  sera  zake  kali  dhidi ya  wahamiaji, aliingilia katika  mjadala  wa  Ujerumani jana kwa kuandika   katika  ukurasa  wa  Twitter akikosoa  sera za  Merkel  za kufungua  mipango kwa  wahamiaji, kwamba  ni  makosa  makubwa, kwamba sera  hizo  zimechochea  uhalifu  barani  Ulaya. Kiongozi wa  chama  cha  CSU, Horst Seehofer,  alikubali  mjini  Munich kuchelewesha  kuweka  marufuku   ya  kuingia  katika  jimbo  hilo hadi  baada  ya  mkutano  wa  kilele  wa  Umoja  wa  Ulaya  tarehe 28  hadi  29  Juni, kumpa  muda  zaidi   Merkel  kutafuta  suluhisho  la jumla  kwa  mataifa  ya  Umoja  huo.

München Seehofer PK nach CSU-Präsidiumssitzung
Waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer wa chama cha CSUPicha: Reuters/R. Orlowski

Merkel anapinga  hatua  yoyote  ya  peke  yake inayoweza kuchukuliwa  na  waziri  wa  mambo ya  ndani  Horst Seehofer, ambaye ni  mwenyekiti  wa  chama  cha  CSU, ambayo  itabadilisha sera yake  ya  kufungua  milango  kwa  wahamiaji  ya  mwaka  2015 na  kudhoofisha mamlaka  yake.

Maadili  ya  pamoja Ulaya  na  Marekani

Ulaya  na  Marekani  hazina  maadili  ya  pamoja, msemaji  wa serikali  ya  Ufaransa  amesema  leo  wakati  hasira  ikiongezeka kuhusiana  na  sera  ya  utawal  wa  rais Trump  ya  kuwatenga wazazi  wahamiaji  na  watoto  wao  wanaowasili  kutoka  katika mpaka  na  Mexico.

Singapur Donald Trump Pressekonferenz
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: Reuters/J. Ernst

Mtafaruku   kuhusiana  na  watoto  waliowekwa  kizuwizini unatokana  na  sera  za  rais  Donald Trump  za  kutovumilia  kabisa wahamiaji, ambamo  wahamiaji  wanakamatwa  wanapoingia Marekani  kinyume  na  sheria  na  wanashitakiwa  kwa  uhalifu.

Seneta  wa  Marekani Ted Cruz  kutoka  jimbo  la  Texas amezungumzia  kuhusu  sakata  hilo  nchini  Marekani, hali  ambayo inaleta  mtafaruku  duniani.

"Sisi  wote ambao  tumeona picha za  watoto wakiondolewa  kwa mama na  baba  zao wakilia, tunajisikia  vibaya sana. Hali hii  ni lazima isitishwe. Wiki  hii  nitawasilisha  mswada  wa  sheria  ambao unawalinda  watoto  na  wazazi  wao  ambao  utawala  ammlaka watoto  kuishi  na  wazazi  wao. Na  pia  utaondoa  mashitaka. Sababu  ya  haya  kutokea  ni  kwamba kuna kesi  nyingi  za uhamiaji."

USA Ted Cruz
Seneta wa jimbo la Texas Ted CruzPicha: picture alliance/AP Photo/D. Cummings

Kansela  Angela  Merkel atakuwa  na  mkutano  leo   na  rais  wa Ufaransa  Emmanuel  Macron kwa  mazungumzo  ya  pamoja kuhusiana  na  mageuzi  ya  Umoja  wa  Ulaya, hususan  masuala muhimu  ya  uhamiaji  ambayo  yanaligawa  kundi  hilo  la  mataifa na  kuweka  mbinyo katika  siasa  za  ndani  ya  Ujerumani  kwa Markel.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Josephat Charo