1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Biashara

Mzozo wa uuzaji miraa kati ya Kenya na Somalia

Shisia Wasilwa, Dw, Nairobi.3 Agosti 2020

Wafanyibiashara wa mirungi au miraa nchini Kenya wameilaumu serikali ya Puntland nchini Somalia kwa kuirejesha ndege iliyokuwa imebeba bidhaa hiyo kwa madai ya kukiuka masharti ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.

https://p.dw.com/p/3gLdZ
Bildergalerie Khat Verbot in Großbritannien Lage in Somalia
Picha: Reuters

Hii ni mara ya pili kwa Somalia kuzuia ndege ya mirungi kutoka Kenya kutua katika ardhi yake kwa kipindi cha mwezi mmoja. Mapema mwezi Julai, ndege iliyokuwa na tani 13 za bidhaa hiyo ilikataliwa kuingia nchini humo kwa madai ya kukosa kuzingatia masharti na kanuni za kukabiliana na virusi vya corona.

Somalia inasema kuwa haijafungua anga yake kwa safari za ndege za kimataifa, hivyo kurejesha ndege hiyo nchini Kenya. Huenda hatua hiyo ikaibua mzozo wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo, ambayo yana historia ya kuzozana.

Mwenyekiti wa chama cha wafanyibiashara wa Miraa nchini Kenya, Kimathi Munjuri amekosoa hatua hiyo ya Somalia na kudai kuwa ni hujuma kwa wakulima na wafanyibiashara kwa jumla.

Wafanyabishara wailaumu serikali ya Kenya kwa kutousuluhisha mzozo

Wafanyabiashara wa miraa nchini KEnya waishutumu serikali kwa kutoushughulikia mzozo kuhusu miraa kati ya Kenya na Somalia ipasavyo.
Wafanyabiashara wa miraa nchini KEnya waishutumu serikali kwa kutoushughulikia mzozo kuhusu miraa kati ya Kenya na Somalia ipasavyo.Picha: Reuters

Wafanyibiashara hao wameilaumu serikali ya Kenya kwa kile wanachokitaja kuwa ni kujikokota kuwasiliana na serikali ya jimbo la Puntland kuhusu uamuzi huo wake. Wizara ya mambo ya nje nchini Kenya haijatoa taarifa yake.

Somalia ilisitisha biashara ya Mirungi mwezi Machi mwaka huu kama sehemu ya hatua za kukabiliana na kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona. Ndege iliyozuiliwa ilikuwa inaelekea katika jimbo la Puntland na ilikuwa imebeba tani 11 za miraa.

Kenya imekuwa ikiuza tani 50 za miraa kwa Somalia yenye thamani ya shilingi milioni 25 za Kenya kila siku. Wafanyibiashara hao wamelaumu wizara ya Mambo ya nje ya Kenya kwa mwendo wao wa kobe wa kusuluhisha mgogoro huo.

Maandamano Hergesia kufuatia ndege iliyobeba miraa kuzuiwa

Baadhi ya nchi ikiwemo Uingereza, Marekani na nchi za Ulaya zimeipiga marufuku biashara ya miraa, kwa kuitizama kuwa dawa ya kulevya.
Baadhi ya nchi ikiwemo Uingereza, Marekani na nchi za Ulaya zimeipiga marufuku biashara ya miraa, kwa kuitizama kuwa dawa ya kulevya.Picha: AP

Katika eneo la Hergeisa, ambapo bidhaa hiyo ilikuwa ikipelekwa watumiaji wa mirungi  walikuwa wakiandamana baada ya ndege ya Kenya kuzuiliwa. Jimbo hilo linakabiliwa na uhaba wa bidhaa hiyo baada ya mzozo kutokea katika jimbo la Oromia nchini Ethiopia.

Uingereza, Marekani na mataifa ya Ulaya ambapo bidhaa hiyo ilikuwa ikiuzwa ilipigwa marufuku kwa kuitaja kuwa ni dawa ya kulevya. Wanaofanya biashara hiyo sasa walikuwa wamesalia na taifa la Somalia kama soko pekee. Inakadiriwa kuwa watu nusu milioni hupanda mirungi katika upembe wa Afrika.

Mwaka 2019 biashara ya mirungi kati ya Kenya na Somalia ilipata pigo baada ya mzozo wa kidiplomasia wa mpaka kati ya mataifa hayo kuibuka, huku wafanyibiashara wa Somalia wakigoma kununua miraa kutoka Kenya.