1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani awataka viongozi Kenya kukaa meza moja.

13 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CouC

Nairobi.Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika Jendayi Frazer amewataka viongozi mahasimu nchini Kenya kutambua kuwa kulikuwa na mapungufu katika uchaguzi nchini humo ambayo yamesababisha kuzuka kwa ghasia na kuachana na masharti ya kabla ya kufanyika mazungumzo.

Naibu waziri huyo amesema katika taarifa kuwa ni muhimu kwa rais Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kukaa pamoja kwa mazungumzo ya ana kwa ana bila masharti.

Odinga anasisitiza kuwa amepokonywa ushindi katika uchaguzi mkuu wa rais mwezi uliopita, na amekataa kutambua kuchaguliwa tena kwa rais Kibaki ama kukaa meza moja hadi pale atakapokiri kuwa kulikuwa na wizi katika uchaguzi. Akisisitiza kuendelea kufanyika maandamano Odinga amesema.

Hadi pale watakapokuwa tayari kuja katika meza ya majadiliano watu wetu wataendelea na maandamano. Kwa sababu hii ndio njia pekee ambayo iko katika uwezo wetu, ambapo tunaweza kuonyesha kutoridhishwa kwetu pamoja na hasira zetu dhidi ya wizi wa kura.

Kibaki jana Jumamosi amesisitiza umuhimu wa viongozi wa kisiasa kuwahudumia Wakenya wote. Ghasia ambazo zilifuatia kuapishwa kwa Kibaki hapo Desemba 30 zimesababisha kupotea kwa maisha ya watu 600 na wengine 250,000 kupoteza makaazi yao, huku umoja wa mataifa ukionya kuwa watu nusu milioni watahitaji msaada wa kiutu katika wiki zijazo.