1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nairobi. Kenya yajadili sekta yake ya sukari.

28 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBxW

Kenya inafanya mazungumzo na jumuiya ya soko la mashariki na kusini mwa Afrika COMESA juu ya kurefusha muda wa hadhi maalum inayotolewa kwa sekta ya sukari katika nchi hiyo , iliyotolewa miaka minne iliyopita.

Hii ni kutokana na hofu kuwa wazalishaji wa sukari nchini humo hawataweza kupambana na ushindani wa wazi na wenzao katika kundi hilo la kibiashara wakati muda huo utakapomalizika March mwakani.

Hadhi maalum ilitolewa ili Kenya iweze kufanyia mageuzi viwanda vyake vya sukari ili kuifanya sukari inayozalishwa nchini humo kuweza kushindana katika soko, hususan na sukari kutoka Malawi, Mauritius na Sudan.

Chini ya makubaliano hayo , Kenya inaruhusiwa kuzuwia uingizaji nchini wa sukari kutoka mataifa mengine ya Comesa kwa kiasi cha tani 200,000 kwa mwaka , kiasi ambacho ni pungufu kati ya uzalishaji wa wastani ndani ya nchi na matumizi.