1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI: Kenya yakosolewa kwa kuwafukuza wasomali

20 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CPau

Makundi ya kutetea haki za binadamu yameikosa vikali Kenya kwa kuwafukuza wakimbizi 18 wasomali, ambao tayari walikuwa wamekataliwa nchini Uganda licha ya hali mbaya ya usalama nchini mwao.

Mwenyekiti wa jukwaa linapopigania haki za waislamu, Ali Amin Kimanthi, amewashutumu maafisa wa polisi nchini Kenya kwa kuwapiga baadhi ya wakimbizi hao, wakati walipokuwa wakiingizwa katika ndege kurudishwa Mogadishu.

Shirika la Umoja wa Mataifa linawashughulikia wakimbizi, UNHCR, limesema limekatazwa kukutana au kuwahudumia wakimbizi 50 ambao wamekuwa wakizuiliwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, tangu walipofukuzwa kutoka Uganda mnamo tarehe 12 mwezi huu.

Msemaji wa shirika hilo mjini Nairobi, Emmanuel Nyabera, amesema walijaribu kuwafikia wakimbizi hao lakini wakaambiwa sharti wapate kibali kutoka kwa wizara ya uhamiaji.

Kamanda wa polisi katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, Joseph Mumira, amesema wasomali hao hawakufukuzwa bali wamerudishwa nchini kwao.