1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani atafadhili ujenzi mpya wa Gaza?

Sudi Mnette
14 Desemba 2023

Tathmini ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa takribani majengo 40,000 au asilimia 18 ya majengo yaliyokuwepo kabla ya kuzuka kwa vita katika Ukanda wa Gaza yameharibiwa katika eneo hilo tangu vita vilipoanza Oktoba 7.

https://p.dw.com/p/4a8FE
Gazastreifen | Die israelischen Angriffe auf Gaza gehen weiter
Maeneo ya mji wa Gaza ambayo majengo yake yamevunjwa na makombora ya IsraelPicha: Mahmoud Sabbah/picture alliance

Hata wakati mapigano, vifo na uharibifu vikiendelea, hoja kuhusu fedha zimekwishaanza. Idadi ya vifo katika mzozo wa Gaza haihesabiki, lakini siyo gharama za ujenzi mpya wa kile kilichoharibiwa kupitia mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza. Makadirio ya awali yanaonyesha zinaweza kufikia hadi dola bilioni 50.

Wiki hii, vyombo vya habari nchini Israel viliripoti kuwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu aliwaambia wanasiasa wenzake kwamba Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zingekuwa tayari kulipia gharama za ujenzi mpya wa Gaza.  Imeelezwa pia kuwa Umoja wa Ulaya utakuwa tayari kulipia.

Umoja wa Ulaya, na hasa Ujerumani na juhudi ya ufadhili katika maeneo yanayokaliwa

Umoja wa Ulaya, na hasa Ujerumani, zimekuwa wafadhili wakubwa wa muda mrefu wa msaada wa kiutu katika maeneo yanayokaliwa ya Wapalestina. Marekani ni mmoja ya wafadhili wengine wakubwa na yenye uwezekano wa kuombwa kufadhili ujenzi mpya.

Lakini ndani ya Marekani na Ulaya, wajuzi wa mambo wanaripoti kwamba nyuma ya pazia, watoa maamuzi tayari wanahoji kwa nini watoe mamilioni ya fedha za walipa kodi kujenga upya miundombinu ambayo itakuja kulipuliwa katika wakati mfupi ujao.

Mchambuzi wa masuala ya kigeni wa gazeti la Financial Times la Uingereza, Gideon Rachman, aliandika wiki hii kwamba amesikia maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya wakisema wazi kwamba Ulaya haitalipia ujenzi mpya wa Gaza, wakati ambapo kiasi cha pesa kinachotakiwa na Ukraine tayari kinawatia kiwewe. "Bunge la Marekani Congress, pia linaonekana kupinga aina zote za msaada wa kigeni.

Miito ya ujenzi mpya wa Gaza, wakati uharibifu unaendelea

Nahostkonflikt - Rafah
Mmoja kati ya wakazi amesimama mbele ya nyumba yake iliyoharibiwa huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.Picha: Mohammed Abed/AFP

Kumekuwa na miito kwa Israel kulipia uharibifu iliyoufanya wakati wa kampeni yake ya sasa huko Gaza, huku baadhi wakihoji kwamba kwa sababu Israel inachukuliwa na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na mashirika ya kimataifa kuwa taifa la ukaliaji huko, inapaswa kubeba jukumu la kuijenga upya Gaza.

Mnamo mwaka 2010, Israel ilikubali kulifidia shirika kuu la Umoja wa Mataifa linalofanya kazi Gaza - la UNRWA, kiasi cha dola za Marekani milioni 10.5 kwa ajili ya majengo yalioharibiwa waakti wa operesheni yake ya mwaka 2009 katika ukanda huo.

Hili lilikuwa suala tata kwa Waisrael, waliohoji iwapo malipo hayo yalimaanisha kuwa wanakiri makosa, na mashirika ya haki za binadamu, yaliosema fedha zaidi zilipaswa kulipwa kwa waathirika. Hata hivyo huo unaonekana kuwa wakati pekee ambapo Israel ilikubali kulipa fidia.

Hali ya mashambulizi ndani ya Gaza yenye wakazi zaidi ya milioni

Tangu Hamas ilipofafanya uvamizi nchini Israel Oktoba 7, Israel imekuwa ikiishambulia Gaza yenye wakaazi zaidi ya milioni. Hamas inaainishwa kama kundi la kigaidi na Ujerumani, Umoja wa Ulaya, Marekani na wengine. Israel imefanya mashambulizi ya ardhini ndani ya Gaza, na inazuwia ufikishaji wa chakula, maji, umeme na sehemu kubwa ya msaada huko, huku mapigano yakiendelea.

Matokeo yake ni kwamba zaidi ya nusu ya nyumba za Gaza zimeharibiwa - hadi makazi 50,000 yamevunjwa na zaidi ya 200,000 kuharibiwa. Zaidi ya hapo, hospitali kadhaa, mamia ya shule na majengo ya serikali, zikiwemo maktaba, makavazi na majengo ya manisaa, yameharibiwa, pamoja na maeneo ya kilimo. Sehemu kubwa ya majengo hayo iligharamiwa na ufadhili kutoka kwa wahisani.

Soma zaidi:Israel yaendelea na mashambulizi Gaza licha ya ukosoaji wa Marekani

Baada ya mashambulizi ya mwisho ya Israel dhidi ya Gaza mwaka 2021, karibu nyumba 1,000 na majengo ya biashara yalivunjwa, na mengine zaidi ya 16,257 kuharibiwa, pamoja na shule 60. Gharama ya ujenzi mpya ilikuwa karibu dola bilioni 8. Sasa nani atagharamia bili kubwa na inayoendelea kuongezeka safari hii?

Jibu ni gumu kwa sababu ufadhili wa msaada na ujenzi mpya wa Gaza, pamoja na maeneo yanayokaliwa ya Wapalestina na miradi mingine inayohusiana na Palestina, limekuwa suala gumu kisiasa kwa miongo kadhaa. Utata huo hautarajiwi kuisha kwa sababu tu ya uhitaji mkubwa na uharibifu wa kipekee uliosababishwa na vita hivi, anasema Nathana Brown, kutoka Programu ya Mashariki ya Kati ya Mfuko wa Carnegie. Kimsingi, anasema hali itakuwa mbaya zaidi.

Chanzo: RTR