1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani ataizuia Bayern Munich msimu huu?

9 Agosti 2013

Nani ataweza kuizuwia Bayern Munich msimu huu, hilo ni swali ambalo timu nyingine katika Bundesliga zinapaswa kulijibu. Jambo ambalo liko wazi ni kuwa, Guardiola atakuwa na mbinyo

https://p.dw.com/p/19N6y
Spain's soccer player Thiago Alcantara (R) and Bayern Munich's head coach Pep Guardiola pose during the official presentation of Bayern Munich's new player at the training area in Munich July 16, 2013. REUTERS/Michaela Rehle (GERMANY - Tags: SPORT SOCCER)
Deutschland Fußball Thiago Alcantara Vorstellung bei FC Bayern München mit Pep GuardiolaPicha: Reuters

Hii ni kwa sababu aliwapata wachezaji anaowataka katika kikosi hicho Mario Goetze kutoka Borussia Dortmund na Thiago Alcantara kutoka Barcelona. Sasa ni wakati wa kuleta mataji. Ama sivyo hali inaweza kuwa mbaya.

"Kuwa juu ni jambo moja na kuendelea kuwa juu ni jambo lingine. Hilo ndio jambo gumu zaidi kwa kazi ya kocha ," amesema rais wa Bayern Munich Uli Hoeness, ambaye pia amemsifu kocha huyo. Iwapo hataweza kufanikisha changamoto hii, nani ataweza? ameuliza Hoeness.

Mario Götze aliwaghadhabisha mashabiki wa Dortmund kwa kujiunga na mahasimu Bayern
Mario Götze aliwaghadhabisha mashabiki wa Dortmund kwa kujiunga na mahasimu BayernPicha: picture-alliance/dpa

Kocha wa makamu bingwa Borussia Dortmund Jurgen Klopp hasemi sana lakini kocha huyo anapaswa kutafuta njia mpya ya kuisaidia timu yake kumeza machungu ya kufungwa na Bayern katika fainali ya kombe la Champions League, na pia kuondoka kwa mchezaji nyota na chipukizi Mario Goetze kwenda Bayern.

Lakini Klopp tayari ameanza kukisifu kikosi chake. Kikosi hicho kiliinyoa bila maji mwishoni mwa mwezi uliopita Bayern Munich katika mchezo wa Super Cup wa kufungua pazia la msimu huu. Dortmund haijasajili wachezaji nyota wa kimataifa , lakini imepata silaha mpya kama Henrikh Mkhitaryan , Pierre-Emerick Aubameyang na Sokratis. Na kocha wa Borussia Dortmund anaamini bado kuwa timu hiyo inaweza kuipa Bayern Munich changamoto kubwa.

Bayer Leverkusen na Schalke 04 ni timu mbili nyingine ambazo wadadisi wa masuala ya soka wanaamini kuwa zinaweza kupambana na Bayern na Dortmund.

Henrikh Mkhitaryan atakosa mechi za mwanzo za BVB
Henrikh Mkhitaryan atakosa mechi za mwanzo za BVBPicha: picture-alliance/dpa

Dortmund ambao walishinda taji la mwaka wa 2011 na 2012, wameanza msimu bila nyota wao waliyemsajili msimu huu Henrikh Mkhitaryan, ambaye ana jeraha la kifundo, wakati Ilkay Gundogan akitiliwa shaka kucheza kutokana na matatizo ya mgongo. BVB wanakutana ugenini na Augsburg.

Bayer Leverkusen, ambayo ilimaliza ya tatu msimu uliopita, inafungua kampeni yake nyumbani leo dhidi ya Freiburg, ambayo ilimaliza katika nafasi ya tano licha ya kutokuwa na raslimali nyingi

Eintracht Frankfurt, iliyomaliza pointi sawa na Freiburg, inafungua dimba leo dhidi ya wageni Hertha Berlin, ambao wamerudi katika Bundesliga baada ya kuwa nje kwa mwaka mmoja.

Pia Jumamosi, Hoffenheim wanawaalika Nuremberg wakati Wolfsburg wakisafiri nyumbani kwa Hannover. Wageni wengine wa Bundesliga Eintracht Braunschweig, ambao wamerudi baada ya kuwa nje kwa miaka 28, wanawaalika Werder Bremen, amba wanaanza msimu mpya katika miaka 14 bila kocha Thomas Schaaf. Mainz inawaalika Stuttgart Jumapili wakati Schalke 04 wakipemenyana na wenyeji Hamburg SV, klabu pekee ambayo haijawahi kushushwa daraja kutoka Bundesliga.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman