1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani kuwa mwenyeji michuano ya kombe la mataifa ya Afrika?

Sylvia Mwehozi
2 Januari 2019

Shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika CAF wiki ijayo, linatarajiwa kumtangaza mwenyeji wa mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika yaliyopangwa kufanyika mwezi Juni-Julai mwaka huu.

https://p.dw.com/p/3Av02
Werbeball für den Afrika-Cup 2010
Picha: picture-alliance/dpa/B. Fonseca

Hatua hiyo ni baada ya Cameroon kupokonywa haki hiyo kwasababu ya maandalizi mabaya na kukosekana kwa usalama. 

Mashindano hayo ya kombe la mataifa ya Afrika yatafanyika kwa mara ya kwanza baada ya kubadilishwa tarehe na pia kuongezeka kwa timu kutoka 16 hadi 24. Lakini hadi sasa mwenyeji wa mashindano hayo hajajulikana. Awali michuano hiyo ilikuwa ikifanyika kati ya mwezi Januari na Februari, lakini hali hiyo iliwapatia wakati mgumu wachezaji maarufu wa kiafrika kuondoka katika timu wanazozichezea barani Ulaya. Kuongezwa kwa timu shiriki pia tayari kumeongeza chachu ya mashindano, timu za Madagascar na Mauritania zimefuzu kushiriki michuano hiyo.

Mchezaji maarufu wa Liverpool na raia wa Misri, Mohamed Salah huenda akaendeleza ubabe wa kuwa mchezaji bora wa Afrika hapo Januari 8 mjini Dakar, sambamba na Sadio Mane wa Senegal ambaye ni mshindani wake. Kama Salah ataendelea kupachika magoli mfululizo, anaweza pia kuvunja rekodi ya nyota wa zamani wa Ivory Coast na Manchester City Yaya Toure, ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora kwa mara nne mfululizo.

Africa Cup Fußball | Marokko vs. Kamerun
Wachezaji wa timu ya Morocco wakifurahia ushindi dhidi ya CameroonPicha: Getty Images/AFP/F. Senna

Kuna machache ya kuchagua kati ya Misri au Afrika Kusini kama mwenyeji wa michuano. Zote hizo mwanzoni hazikuwa kwenye maombi ya awali kuyaandaa. Lakini kuna utofauti kidogo wa hali ya hewa, Misri itakuwa kwenye kipindi cha majira ya joto kaskazini mwa Afrika wakati Afrika Kusini kipindi hicho kitakuwa cha baridi kali.

Ikiwa Misri itachaguliwa kuwa mwenyeji, bingwa huyo wa mara saba wa Afrika atakuwa na nafasi nzuri ya kufanya vyema kuliko mwaka 2017 wakati alipobwagwa fainali dhidi ya Cameroon huko Libreville. Ikiwa Afrika Kusini naye atakuwa mwenyeji, ni kwamba Senegal na mabingwa wa zamani Tunisia, Morocco na Nigeria watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kunyanyua kombe.

Mshindi wa michuano ya klabu bingwa Afrika kwa mwaka uliopita Esperance ya Tunisia, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Al Ahly ya Misri, zimeshinda mara saba katika fainali 10 zilizopita na ambazo zinapewa kipaumbele. Al Ahly, chini ya kocha mpya kutoka Uruguay Martin Lasarte, itakuwa na shauku ya ushindi tangu mwaka 2013 ilipopoteza fainali mbili dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco na Esperance.

Klabu za Kaskazini ya Afrika zimeshinda mara 10 kwenye fainali 15 ya mashindano. Klabu ya Raja Casablanca ya Morocco ni timu iliyo na nguvu katika ukanda huo. Lakini wapo wanaozitupia macho klabu nyingine mbali na Raja, kama vile Etoile Sahel, CS Sfaxien ya Tunia na Zamalek ya Misri.

UK Mohamed Salah
Nyota wa Liverpool na mchezaji wa timu ya Misri Mohamed SalahPicha: imago/Action Plus/D. Blunsden

Kubadilishwa kwa tarehe ya michuano ya klabu bingwa kutoka mwezi Agosti hadi Mei mwaka huu, pia kutatoa muda mzuri wa maandalizi. Siku za mwanzo za mwezi Machi zitatumiwa kuhitimisha michezo ya kufuzu mashindano hayo na kuna siku nyingine tisa za ziada kwa ajili ya dirisha la kimataifa katika nusu ya mwaka. Je Afrika itazingatia kufuata mwelekeo wa Ulaya wa kuanzisha ligi ya mataifa ya Afrika? Itakuwa ni mafanikio kwa mechi za kirafiki za kiafrika ambazo wakati mwingi zinaepukwa na wachezaji maarufu wanaokipiga klabu za Ulaya.

Algeria, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini na Misri zilifuzu mashindano mawili yaliyopita lakini ziliwekwa kando katika raundi ya tatu ya mtoano katika michuano. Hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusiana na kufuzu kwa mashindano hayo pekee ya kimataifa hasa kwa wachezaji wanaochezea katika nchi zao za asili.

Ethiopia itaandaa fainali za mwaka 2020, ikiwa ni mara ya kwanza kwa taifa la mashariki mwa Afrika kuandaa mashindano ya CAF tangu ilipoyaandaa mnamo mwaka 1976.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/afp

Mhariri: Mohammed Khelef