1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yahakikisha kukamilisha operesheni Libya

18 Aprili 2011

Huku mashambulio makali vikosi vya Muammar Gaddafi yakiripotiwa katika mji wa Misrata, Jumuiya ya Kujihami ya NATO imesema kwamba ina uhakika wa kuongeza ndege za kijeshi kwa ajili ya operesheni yake nchini Libya.

https://p.dw.com/p/10vgp
Bomu la mchawanyiko
Bomu la mchawanyikoPicha: AP/Human Rights Watch

Afisa wa ngazi ya juu wa NATO ameliambia Shirika la Habari la Associated Press kwamba, Jumuiya yake ina uhakika kuwa mashambulio mengine tisa tu yatatosha kuifanisha operesheni yao nchini Libya.

Afisa huyo, ambaye amekataa kutajwa jina lake kwa sababu za kitifaki, amesema kwamba NATO inatarajia kupata ndege zaidi za kijeshi kufanya mashambulizi hayo dhidi ya vikosi vya Gaddafi. Afisa huyo amesema kuwa NATO ina silaha za kutosha kutekeleza jukumu lake.

Lakini, wakati NATO ikijiaminisha kuwa na nguvu za kutosha kuendeleza kampeni yake nchini, taarifa kutoka mji wa Misrata zinasema kwamba maelfu ya watu wamekwama katika mji uliozingirwa na vikosi vya Gaddafi.

Vifo zaidi Misrata

Bango linalompinga Gaddafi
Bango linalompinga Gaddafi

Madaktari wanasema kiasi ya watu 17 waliuawa hapo jana pekee, na wengine kadhaa wakijeruhiwa, huku kukiwa na taarifa za kutumika mabomu hatari ya mchawanyiko.

Daktari mmoja wa Misrata amesema kwamba mabomu haya yamekuwa yakiwahasiri vibaya raia wa kawaida, wakiwamo wanawake na watoto

"Mimi na mwenzangu tumewaona majeruhi wa mabomu ya mchawanyiko, hata mpiga picha wa televisheni ya Kifaransa alikuwa mmoja wa wahanga wa mabomu hayo. Wahanga wengi ni watoto, ambao wana majeraha vifuani, tumboni na machoni." Amesema daktari huyo.

Meli iliyopelekwa na Shirika la Wahamiaji la Kimataifa, IOM, hapo jana kuwaokoa wageni waliokwama, imeondoka kuelekea mji wa Benghazi ikiwa na wageni 1,000 tu, na baadhi ya majeruhi wa Kilibya, kati ya kiasi ya raia 400,000 walioganda kwenye mji huo.

Shirika hilo linasema kwamba uwezo wake wa kuwaokoa watu ni mdogo kulinganisha na mahitaji yaliyopo. Miongoni mwa wageni waliookolewa ni wale wa Ghana, Ufilipino na Ukraine.

NATO imetuma takribani ndege 200 kwenye operesheni yake dhidi ya vikosi vya Gaddafi, tangu ianze karibuni mwezi mzima sasa. Lakini, kwa siku za hivi karibuni, kumekuwapo na hali ya msuguano miongoni mwa wanachama wenyewe wa NATO, kwa upande mmoja, na waasi na NATO, kwa upande mwengine, juu ya kasi na ufanisi wa operesheni hii, panapohusika azma ya kuwalinda raia.

Afrika Kusini yafungua tena ubalozi

Rais wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma
Rais wa Afrika ya Kusini, Jacob ZumaPicha: picture-alliance/dpa

Katika hatua nyengine, serikali ya Afrika ya Kusini imeufungua tena ubalozi wake mjini Tripoli, katika jitihada za kumtafuta mwandishi wa habari aliyepotea.

Mwandishi huyo, Anton Hammerl, alipotea tarehe 7 mwezi huu, akiwa na wenzake wawili wa Kimarekani na mmoja wa Kihispania. Serikali ya Afrika ya Kusini imekuwa ikishinikizwa na mashirika ya ndani na nje, itumie ushawishi wake kwa serikali ya Libya, ili kusaidia kuachiwa kwa Hammerl.

Rais Jacob Zuma, ambaye leo hii aliongea kwa simu na Gaddafi, amekuwa akilaumiwa kwa kutokutumia fursa ya wiki iliyopita alipozuru Libya, kuzungumzia suala la Hammerl.

Zuma ni miongoni mwa wajumbe wa jopo la maraisi wa Umoja wa Afrika walioteuliwa kutafuta amani ya Libya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman