1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Guterres aitaka China kuruhusu Mkuu wa Haki kuzuru Xinjiang

Daniel Gakuba
5 Februari 2022

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewaambia viongozi wa China kuwa anatumai watamruhusu mkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet kufanya ziara katika jimbo la Xinjiang.

https://p.dw.com/p/46aSv
Peking Olympische Winterspiele | IOC-Präsident Thomas Bach und Xi
Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres (kushoto), akimsalimia Rais Xi Jinping wa China (wa 3 kutoka kushoto) kwenye michezo ya Olimpiki mjini BeijingPicha: TOBIAS SCHWARZ/AFP

Guterres amekutana na Rais Xi Jinping wa China na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Wang Yi pembezoni mwa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi mjini Beijing.

Soma zaidi: Michezo ya Olimpiki msimu wa baradi yaanza rasmi Beijing

Tangazo kutoka mkutano wa viongozi hao limesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa '' ameelezea matumaini yake kwamba mawasiliano kati ya ofisi ya Kamishna wa Haki za Binadamu na maafisa wa serikali ya China, yataruhusu ziara 'yenye kuaminika' ya kamishna huyo nchini China, ikiwa ni pamoja na jimbo la Xinjiang.''

Taarifa ya shirika la habari la serikali ya China, Xinhua kuhusu mkutano huo na Guterres, haikusema chochote kuhusu suala hilo la haki za binadamu.

Schweiz Genf | UN-Hochkommissarin für Menschenrechte zu Äthiopien, Tigray
Licha ya maombi ya muda mrefu, mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet hajaruhusiwa kulizuru jimbo la Xinjiang bila vikwazoPicha: Denis Balibouse/REUTERS

Shutuma nzito za wanaharakati

Watetezi wa haki za binadamu wanasema kuwa watu wasiopungua milioni moja kutoka jamii ya Waislamu walio wachache, wamelazimishwa kuishi katika ''kambi za mafunzo'' jimboni Xinjiang lililo magharibi mwa China, wakiituhumu China kwa uhalifu mkubwa wa haki za binadamu, unaohusisha kuwafunga kizazi wanawake wa jamii hiyo, na kazi za shuruti.

Soma zaidi: China yamulikwa kwa ukiukaji wa haki za binaadamu

Mnamo siku zilizotanguliwa kufunguliwa rasmi kwa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi mjini Beijing, wizara ya mambo ya nje ya China ilisisitiza katika mikutano yake ya kila siku na waandishi wa habari, kuwa Guterres anaiunga mkono michezo hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa binafsi amempongeza rais Xi kwa kuiandaa michezo hiyo walipokutana mjini Beijing, imeeleza taarifa ya Umoja wa Mataifa.

Eröffnungsfeier | Olympische Winterspiele 2022 | Peking, China
Dinigeer Yilamujiang (kushoto), mwanariadha kutoka jamii ya Uyghur alikuwa miongoni mwa walioukimbiza mwenge wa Olimpiki.Picha: EVGENIA NOVOZHENINA/REUTERS

Hata hivyo, hadi  sasa China imemzuia Michelle Bachelet ambaye ni rais wa zamani wa Chile, kufanya ziara iliyo huru katika jimbo la Xinjiang.

China yakanusha kufanya 'mauaji ya halaiki' Xinjiang

Serikali ya Marekani pamoja na mabunge ya nchi nyingine tano za magharibi, wametangaza kuwa inachokifanya China dhidi ya watu wa jamii ya Uyghurs jimboni Xinjiang ni sawa na ''mauaji ya kuangamiza'', tuhuma ambazo China inazikanusha vikali.

Soma zaidi: Rais Vladmir Putin amewasili mjini Beijing.

China vile vile imewaonya wakosoaji wake kuacha kuitumia michezo ya Olimpiki kwa malengo ya kisiasa. Tayari michezo hiyo inafunikiwa na viwingu vya ukiukaji wa haki za binadamu, Covid-19, na hofu juu ya kinachoweza kutokea kwa wanariadha wtakaotoa mawazo yao wakishiriki katika michezo hiyo.

Kwenye sherehe za ufunguzi, China ilimchagua mwanariadha chipukizi kutoka jamii ya Uyghur Dinigeer Yilamujiang kuwa miongoni mwa watu walioukimbiza mwenye wa michezo hiyo, hatua ambayo bila shaka ilikuwa na ujumbe wa wazi kisiasa.

China Xinjiang | mutmaßliches Internierungslager für Uiguren
Wanaharakati wanasema majengo kama hili jimboni Xinjiang hutumiwa kama kambi za kuwapokonya utamaduni wao WauyghurPicha: GREG BAKER/AFP/Getty Images

Ripoti ya Umoja wa Mataifa yacheleweshwa

Wanaharakati na wanasiasa wamekuwa wakisubiri kwa hamu ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu jimboni Xinjiang, kwa matumaini kuwa ingechapishwa kabla ya michezo ya Olimpiki kuanza, lakini mwezi uliopita umoja huo ulisema bayana kuwa isingetangazwa kabla ya michezo hiyo.

Gazeti la South China Morning Post linaloandikwa mjini Hong Kong liliashiria kuwa China ilikubali kuridhia ziara ya Michelle Bachelet, kwa sharti kuwa Umoja wa Mataifa ucheleweshe uchapishaji wa ripoti hiyo ya hali ya haki za binadamu.

afpe