1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Kiafrika zisaidiwe kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa

17 Desemba 2009

Tangu mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa ulipoanza mjini Copenhagen,ilidhihirika kuwa hakutakuwepo malengo ya pamoja kwa wote, kwani maslahi ya wajumbe mkutanoni yanatofautiana sana.

https://p.dw.com/p/L4ul
Ethiopian Prime Minister Meles Zenawi is seen at his offices in the capital, Addis Ababa, Wednesday, Jan. 10, 2007. Zenawi said Wednesday that a U.S. airstrike in Somalia had not killed any civilians and, in his opinion, would not help create an Iraq-style insurgency or hinder efforts to build a peacekeeping force in the country. (AP Photo/Les Nauheus)
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi.Picha: AP

Bara la Afrika linahesabika kama eneo lililoathirika sana kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Kwa mujibu wa jopo la waatalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa IPCC, ifikapo mwaka 2020, watu wapatao milioni 75 hadi milioni 250 huenda wakakosa kupata maji ya kutosha wakati wote, kwa sababu ya hali ya ukame inayoendelea katika bara hilo.

Siku ya Jumatano baadhi ya viongozi wa nchi za Kiafrika walihutubia mkutano wa kilele utakaohudhuriwa na zaidi ya viongozi 110 wa serikali na mataifa mjini Copenhagen. Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi anaeongoza ujumbe wa Umoja wa Afrika katika majadiliano ya Copenhagen alikuwa kiongozi wa kwanza kuhutubia mkutano huo wa kilele. Alisema:

"Sitii chumvi kusema kuwa hii ni fursa nzuri kabisa ya kuinusuru sayari yetu na maangamizi ya mabadiliko ya hali ya hewa yasiokadirika. Huu ni mtihani kutuona iwapo sisi kama jamii tunaweza kuweka kando maslahi ya kibinafsi na kuhifadhi mustakabali wetu wa pamoja."

Mbali na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa, mada nyingine kuu kwa nchi za Kiafrika ni msaada wa fedha. Meles Zenawi amependekeza mpango unaozitaka nchi tajiri zitoe msaada wa Dola bilioni 50 kila mwaka kuanzia mwaka 2015 - na bilioni 100 kwa mwaka, kuanzia 2020, ili nchi masikini ziwe na uwezo wa kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Zimbabwean President Robert Mugabe speaks at a ZANU-PF (Zimbabwe African National Union) gathering in Harare, Zimbabwe Friday, Dec. 11, 2009. Zimbabwe's president says infighting is destroying the party that has kept him in power for nearly three decades. (AP Photo/Str)
Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe.Picha: AP

Hata Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe,nchi ambayo miaka ya hivi karibuni ilikatiwa sana misaada ya fedha kutoka jumuiya ya kimataifa, kwa sababu ya ukiukaji wa haki za binadamu, anadai fedha zaidi kupambana na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa. Mugabe alisema:

"Sisi wenye misitu inayohitajiwa kuhifadhi uhai anuwai, tunastahiki kupewa misaada zaidi ya fedha na fursa ya kujipatia teknolojia ya kuhifadhi mazingira."

Hivi karibuni, wajumbe wa Kiafrika walipinga vikali jaribio la kufanya mageuzi katika Itifaki ya Kyoto inayoziwajibisha nchi zilizoendelea kiviwanda kwa kipindi maalum. Mkataba huo wa mazingira unamalizika mwaka 2012. Kwa maoni ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, nchi za Kiafrika ndio zitakazoumia zaidi ikiwa makubaliano ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa hayatopatikana katika mkutano wa kilele mjini Copenhagen.

Mwandishi: J.Beck/ZPR / P.Martin

Mhariri: Hamidou,Oummilkheir