1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege za Urusi mazoezini karibu na Ukraine

4 Agosti 2014

Jeshi la Urusi limeanzisha mazoezi mapya yanayojumuisha ndege 100 za kivita karibu na mpaka baina yake na Ukraine, huku mapigano makali yakiendelea mashariki mwa Ukraine kati ya jeshi na waasi.

https://p.dw.com/p/1CoJw
Baadhi ya ndege zinazotumiwa na Urusi katika mazoezi Karibu na Ukraine
Baadhi ya ndege zinazotumiwa na Urusi katika mazoezi Karibu na UkrainePicha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa jeshi la anga la Urusi Igor Klimov amesema kwamba mazoezi hayo ambayo yanafanyika katika mikoa ya kati na magharibi, ni ya kwanza katika mfululizo wa mengine kadhaa ambayo yanaazimia kuwianisha operesheni za vikosi vya anga vya nchi hiyo mwaka huu. Msemaji huyo hakuitaja Ukraine, ambako jeshi la serikali na waasi wanaoiunga mkono wanakabiliana katika mapigano.

Klimov amesema ndege za Urusi kama vile chapa Su-27 na MIG-31 pamoja na zile mpya kabisa aina ya Su-34 na Mi-8, Mi-24 na helikopta chapa Mi-28N, zote zitatumiwa katika mazoezi hayo ambayo pia yatahusisha majaribio ya makombora.

Mazoezi haya ya jeshi ya yumkini yatazusha wasiwasi miongoni mwa nchi za magharibi, ambazo zimekuwa zikiishutumu Urusi kusababisha mvutano kwenye mpaka wake na Ukraine na kuwaunga waasi wanaotaka kujitenga kwa sehemu ya mashariki ya Ukraine.

Waasi wakabiliwa na shinikizo

Huku hayo yakiarifiwa mapigano yameongezeka baina ya jeshi la Ukraine na waasi hao wa mashariki. Jeshi la nchi hiyo linawazingira waasi katika miji wanayoidhibiti ya Donetsk na Luhansk, katika operesheni ambayo iliimarishwa baada ya waasi hao kutuhumiwa na nchi za magharibi kuiangusha ndege ya abiria ya shirika la ndege la Malaysia, katika ajali iliyouwa watu wote 298 waliokuwa ndani ya ndege hiyo.

Hivi karibuni jeshi la Ukraine limekuwa likiwazidi nguvu waasi wanaotaka kujitenga
Hivi karibuni jeshi la Ukraine limekuwa likiwazidi nguvu waasi wanaotaka kujitengaPicha: Reuters

Naibu meya wa mji wa Donetsk amesema kwamba mapigano yaliyofanywa katika mitaa yenye makazi ya watu yaliuwa raia sita na kuwajeruhi wengine 13. Watu zaidi ya 1,150 wamekwishauawa katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimedumu kwa miezi mitatu sasa.

Kwa upande mwingine jeshi la Ukraine limesema limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya mizinga, likidai baadhi ya mashambulizi hayo yanatoka upande wa Urusi.

Vita vya muda mrefu

Ingawa serikali mjini Kiev inasema itawashinda waasi hao mnamo siku za hivi karibuni, wachambuzi wameonya kwamba huenda vita hivyo vikachukua muda mrefu, kwa sababu waasi ambao wamekula kiapo cha kupigana hadi wa mwisho wamejichimbia katika miji mikubwa mikubwa.

Waasi nao wameapa kupigana hadi mtu wa mwisho
Waasi nao wameapa kupigana hadi mtu wa mwishoPicha: Reuters

Afisa mmoja wa shirika la usalama wa taifa la Urusi, FSB katika mkoa wa Rostov ulio karibu na mpaka wa Ukraine, amesema wanajeshi 400 wa Ukraine wameomba hifadhi nchini Urusi.

Shirika la habari la Urusi Itar-Tass limemnukuu afisa huyo Vasily Malayev akisema jumla ya wanajeshi wa Ukraine 438 walifika kwenye mpaka wa Urusi wakiomba hifadhi ya ukimbizi.

Mazoezi ya awali ya Urusi karibu ya mpaka wa Ukraine yalifanyika mwezi March yakiwahusisha wanajeshi 8,500 wa vikosi vya mizinga , yalikosolewa na nchi za magharibi.

Mwezi May Urusi ilisema imevirudisha nyuma vikosi vyake, lakini umoja wa kujihami - NATO mwezi uliopita liliishutumu Urusi kurundika tena wanajeshi na silaha karibu na mpaka baina yake na Ukraine.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE

Mhariri: Josephat Charo