1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu asema Iran inataka kuiangamiza Israel

Saumu Mwasimba
5 Juni 2018

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu asisitiza hatua zichukuliwe kuizuia Iran isitengeneze silaha za nyuklia. Msimamo wake kuelekea Iran unapingwa barani ulaya anakofanya ziara yake.

https://p.dw.com/p/2yyPn
Frankreich Emmanuel Macron und Benjamin Netanyahu in Paris
Picha: Getty Images/AFP/L. Marin

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema mpango wa Iran wa kuongeza kiwango cha urutubishaji madini ya urani unalenga kutengeneza silaha za nyuklia zitakazotumiwa dhidi ya Israel. Netanyahu yuko Ufaransa anakokutana na Rais Emmanuel Macron, ikiwa ni kituo chake cha pili katika ziara yake Ulaya.

Ziara ya Netanyahu Ulaya inakuja wakati kukiwa na mgawanyiko mkubwa kuhusu jinsi ya kuidhibiti Iran na malengo yake katika Mashariki ya Kati. Leo yuko Paris anakokutana na Rais Macron ikiwa ni mara ya tatu kwa viongozi hao kukutana mjini humo tangu mwezi Julai mwaka jana. Netanyahu na Macron wanakubaliana kwamba miradi ya makombora ya Iran na uingiliaji kati wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu nchi za kigeni ni kitisho, lakini wanatofautiana sana juu ya kuishughulikia nchi hiyo. Netanyahu anasema Iran ni adui na Israel katu haiwezi kuiachia itengeneze silaha za Nyuklia.

Israel Emmanuel Macron & Benjamin Netanjahu
Picha: Reuters/P. Wojazer

''Ayatollah Ali Khamenei alitangaza juzi kwamba nia yake ni kuliangamiza dola la Israel. Jana ameelezea jinsi atakavyofanikisha hilo kwa kuendelea kurutubisha madini ya urani bila kipimo ili kutengeneza silaha  za Nyuklia za maangamizi. Hatukushangazwa. Hatutoiruhusu Iran kutengeneza silaha za nyuklia''

Mgongano kati ya Netanyahu na Macron

Waziri mkuu huyo wa Israel amekuwa akiendelea kuishambulia Iran wakati wa ziara yake barani Ulaya. Akiwa mjini Berlin jana alionya kwamba shughuli za Iran zinahatarisha kuchochea wimbi jipya la wahamiaji kuelekea Ujerumani, akisistiza kwamba Iran inalenga hasa kuchochea vita vya kidini ndani ya Syria na matokeo yake itakuwa ni kumiminika kwa wakimbizi zaidi Ulaya na hususan Ujerumani. Netanyahu amezidi kupata nguvu kutokana na hatua ya Rais Donald Trump ya kuiondowa Marekani katika mkataba wa nyuklia wa 2015 unaoudhibiti mpango wa nyuklia wa Iran.

Iran Ali Khamenei
Picha: Mehr

Lakini Macron ni miongoni mwa viongozi wa Ulaya wanaoutetea kwa nguvu zote mkataba huo uliotiwa saini na nchi yake Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, China, Urusi na Umoja wa Ulaya kwa Ujumla na zote hizo zinaendelea kuunga mkono. Rais Macron na Waziri Mkuu Netanyahu wamepangiwa kuwa na mkutano wa pamoja na waandishi habari baada ya mkutano wao baade na kuzindua msimu wa kubadilishana tamaduni kati ya nchi hizo mbili mwaka huu.

Lakini kinachodhihirika kwa sasa hakuna uhusiano mzuri kati ya nchi hizi mbili na uhusiano huu umezidi kuzorota kutokana na mauaji ya hivi karibuni ya waandamanaji 123 wa Kipalestina huko Gaza katika matumizi ya nguvu yaliyofanywa na wanajeshi wa Israel katika kipindi cha kuanzia mwezi Machi ikiwa ni pamoja na watu 61 waliouliwa mwezi uliopita wa Mei.

Macron alilaani matumizi hayo ya nguvu ya jeshi la Israel, na Waziri Mkuu wa Ufaransa, Edouard Phillipe pia alifutilia mbali ziara ya kwenda Israeli mwezi huo wa Mei. Na kama haitoshi, makundi mbalimbali yanayowaunga mkono Wapalestina yamepanga kuandamana katika miji mbalimbali ya Ufaransa kumpinga Netanyahu, huku vyama vitatu vya waandishi habari nchini humo vikisema ziara yake Ufaransa haikubaliki.

Mwandishi: Saumu Yusuf

Mhariri: Grace Patricia Kabogo