1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu kuapishwa leo

Aboubakary Jumaa Liongo/AFP/DPA31 Machi 2009

Kiongozi wa Chama cha Likud cha mrengo wa kulia, Benjamin Netanyahu anatarajiwa hii leo kuapishwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Israel, kuongoza serikali itakayokuwa na idadi kubwa ya wanasiasa wenye msimamo mkali.

https://p.dw.com/p/HNKD
Kiongozi wa Chama cha Likud Benjamin NetanyahuPicha: AP

Netanyahu ambaye kwa mara ya kwanza miaka kumi iliyopita alishika wadhifa huo, mara baada ya kuapishwa anatarajiwa kuwasilisha majina ya baraza lake la mawaziri bungeni, kabla ya kupigiwa kura mchana huu.


Serikali hiyo mpya inayotarajiwa kutangazwa na Netanyahu na ikiwa ni ya 32 inaitia shaka jumuiya ya kimataifa, kutokana na kugubikwa na mawaziri kutoka vyama vyenye msimamo mkali.


Netenyahu ambaye pia ni maarufu katika duru za kisiasa nchini Israel kwa jina la Bibi, amelazimika kuunda serikali yenye baraza kubwa la mawaziri ili kuwapa nafasi vyama vilivyokubali kujiunga naye kuunda serikali ya mseto.


Waziri Mkuu huyo mteule wa Israel amemteua kiongozi wa chama cha Yisrael Beitenu, Avigdor Lieberman kuwa Waziri wa Nje.Lieberman ambaye aliwahi kuwa mnyanyua vitu vizito na mkimbizi kutoka Jamhuri ya Moldva wakati huo ikiwa katika iliyokuwa Soviet, amekuwa akichukuliwa kuwa ni mbaguzi kutokana na kauli zake.


Kwa kuteuliwa kwake kuchukua nafasi hiyo, pamoja na sera za Netanyahu za kupinga kuanzishwa kwa taifa la Palestina, jumuiya ya kimataifa imeingiwa na wasi wasi juu ya majaaliwa ya maendeleo kidogo yaliyofikiwa katika mpango wa amani ya Mashariki ya Kati uliyofufuliwa miaka miwili iliyopita.


Ehud Barak ambaye ni kiongozi wa chama cha Labour anabakia kuwa Waziri Ulinzi nafasi aliyokuwa nayo katika serikali iliyopita.

Wiki iliyopita, Umoja wa Ulaya ulionya juu ya matokeo yatakayotokea iwapo serikali hiyo mpya ya Israel itashindwa kukubaliana na pendekezo la uundwaji wa mataifa mawili kama njia pekee ya ufumbuzi wa mzozo wa miongo kadhaa katika eneo hilo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa uhusiano utakuwa mgumu sana.


Wakati huo huo Rais Barack Obama wa Marekani amesema kuwa juhudi za amani chini ya serikali ya Netanyahu hazitopata urahisi, lakini akaongeza kuwa ni muhimu.


Netanyahu anapinga kuanzishwa kwa taifa la Palestina uamuzi ambao Israel chini ya makubaliano ya kimataifa ya mwaka 2003 yajulikanayo kama ramani ya barabara kuelekea amani, iliukubali kuutekeleza, na anasema kuwa kabla ya kuendelea kwa mazungumzo ya amani ni lazima kwanza mazingira ya uchumi yaimarishwe katika eneo wanalokalia la Ukingo wa Magharibi


Wakati wa kipindi cha kwanza cha uongozi wake kati ya mwaka 1996 na 1999, Benjamin Netanyahu aliweka kikwazo katika mpango wa amani wa Oslo.


Hata hivyo kutokana na msimamo wa Marekani ambapo Rais Obama amekuwa akilazimisha kuendelea kwa mazungumzo yaliyokwama ya amani, kiongozi huyo mpya wa Israel amesema ataendelea na mazungumzo hayo.


Katika kipindi chake cha kwanza cha uwaziri Mkuu, Netanyahu pamoja na msimamo wake mkali, alitia saini makubaliano kadhaa na Palestina kutokana na mbinyo wa serikali ya Marekani.


Wiki iliyopita Netanyahu alisema kuwa amani ni malengo ya kila mwananchi wa Israel, serikali na yeye akiwemo, kwa maana hiyo amesema, ataendelea kuzungumza na Mamlaka ya Palestina kutafuta amani.


Naye Rais Shimon Perez akijaribu kuitoa wasi wasi jumuiya ya kimataifa, alisema kuwa serikali hiyo mpya itakayoundwa, inawajibika kutekeleza maamuzi yaliyokwishaamuliwa, ambayo ni kuendelea na mazungumzo ya amani.

Mwandishi: Aboubakary Liongo

Mhariri.Mohamed Abdul-Rahman