1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New Zealand yapiga marufuku mauzo ya silaha za kivita

Daniel Gakuba
21 Machi 2019

New Zealand imepiga marufuku mauzo ya bunduki za kivita kama ile iliyotumiwa na mshambuliaji aliuwa watu 50 katika miskiti miwili nchini humo Ijumaa iliyopita, na wanaozimiliki tayari silaha hizo watatakiwa kuzirejesha.

https://p.dw.com/p/3FQ4V
Neuseeland | Waffenshop | Christchurch
Picha: REUTERS

Tangazo la Waziri Mkuu Jacinda Ardern limekuja siku sita baada ya shambulizi katika misikiti miwili mjini Christchurch. Tangu mwanzoni kabisa Bi Ardern ameliita shambulizi hilo kuwa la kigaidi, na kuahidi kuwa sheria za New Zealand zingebadilishwa, kuzuia upatikanaji kirahisi wa silaha zinazoweza kuuwa watu wengi haraka. Kiongozi huyo amesema mauaji hayo yaliibadilisha nchi yake.

''Tarehe 15 Machi, historia yetu ilibadilika milele, na sasa, sheria zetu zitabadilika pia. Leo hii tunatangaza hatua kwa niaba ya wa-New Zealand wote, kuimarisha sheria za umulikaji wa bunduki, ili nchi yetu iwe mahali salama zaidi.'' Amesema Bi Jacinda.

Neuseeland Jacinda Ardern
Jacinda Ardern, Waziri Mkuu wa New ZealandPicha: Reuters/TVNZ

Waziri mkuu huyo alisema ifikapo Machi 11 anatarajia sheria nyingine itapitishwa, kuweka mpango wa wale ambao tayari wanazimiliki silaha zilizopigwa marufuku kuzirejesha serikalini na kupatiwa fidia. Amekadiria kuwa zoezi hilo litaigharimu nchi kiasi cha dola za kimarekani zipatazo milioni 138.

Marufuku pia kwa chemba za ziada

Pamoja na silaha hizo za kivita, vivaa vinavyoziongezea bunduki uwezo wa kubeba risasi nyingi na kufyatua haraka zaidi, pia vimepigwa marufuku. Waziri Mkuu Ardern amesema mtu aliyefanya mashambulizi ya Ijumaa iliyopita aliinunua bunduki yake kihalali, na kisha akaiongezea uwezi kwa chemba ya risasi 30 aliyoinunua kirahisi mtandaoni.

Neuseeland, Christchurch: Beerdigung der Opfer
Mazishi yanaendelea kwa wahanga wa shambulizi la Ijumaa iliyopitaPicha: Reuters/J. Silva

Chini ya sheria ya umiliki wa bunduki iliyokuwepo katika nchi hiyo, kibali cha kawaida kilimruhusu mnunuzi kuwa na uwezo wa kufyatua mfululizo risasi saba tu.

Mojawapo ya maduka makubwa ya kuuza bunduki nchini New Zealand iitwayo Hunting & Fishing New Zealand imesema itaunga mkono hatua yoyote ya serikali kupiga marufuku silaha za kivita. Mkurugenzi wa duka hilo, Darren Jacobs amesema ingawa siku za nyuma walifaidika kwa kuziuza silaha za aina hiyo kwa wateja wachache, tukio la wiki iliyopita limebadilisha mtazamo, na kuwashawishi kuwa silaha za aina ile hazina nafasi katika biashara yao, na katika nchi yao.

Wakulima wakubaliana na serikali

Hatua hiyo ya serikali pia imeungwa mkono na shirikisho la vyama vya wakulima wa nchi hiyo, ambao ndio wamiliki wa sehemu kubwa ya bunduki zilizopo mikononi mwa raia nchini New Zealand.

Huku hayo yakiarifiwa, miskiti itafunguliwa kwa sala ya Ijumaa ya kesho, ambapo pia kutakuwa ibada kubwa ya mazishi ya wahanga wa shambulizi la wiki iliyopita. Baadhi ya waliouwa walizikwa jana na wengine wamezikwa leo. Sala ya kesho katika msikiti wa Al-Noor ambako watu 42 waliuawa, inatarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya watu, wakiwemo watakaotoka katika mataifa ya nje.

rtre,dpae