1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Niedecken Mjini Bonn:Haki na muziki kwenye meza moja

3 Septemba 2010

Wanasiasa, wanauchumi na watu maarufu katika jamii watakapokutana leo Ijumaa mjini Bonn, kujadili misaada ya maendeleo, mwanamuziki wa midundo ya rock, Wolfgang Niedecken atakuwepo miongoni mwao.

https://p.dw.com/p/P3MW
Mwanamuziki Wolfgang NiedeckenPicha: AP

 Kwani ndoto ya mwimbaji huyo wa bendi ya BAP kutoka mji wa Cologne ni kuwa na ulimwengu wa haki na katu hatoachana na ndoto hiyo.Wimbo unaoitwa,"Ingelikuwa Vizuri" unaeleza kuwa hakuna anayelazimika kuwa na njaa,hakuna anaeteseka,hakuna bahili,mwenye nacho atagawa bila ya shaka na hakutakuwepo tena sababu za ugaidi,chuki na kuoneana wivu."

Balozi wa Afrika

Kuna baadhi ya watu wanaomkosoa mwimbaji huyo wa BAP kwa kuwa mtu mwema kupindukia.Lakini hiyo wala haimsumbui. Katika mahojiano yake na gazeti moja miaka michache iliyopita aliuliza, iwapo awe mtu mbaya eti kwa vile wapo wanaokerwa na harakati zake za kupinga dhulma duniani? Mara kwa mara Wolfgang Niedecken ameeleza kwanini hawezi kuachana na mada ya askari watoto na Uganda, hasa kufuatia ziara yake nchini humo katika mwaka 2004. Wakati huo, alikuwa ziarani barani Afrika pamoja na waandishi wa habari kama "balozi kwa bara la Afrika" - Akieleza hisia zake  anasema,''Nilishudia kwa macho yangu mwenyewe huko kaskazini ya Uganda na nikaamua kuishughulikia mada hiyo. Lakini mara ya kwanza kabisa nilikuwepo Msumbiji - hiyo ilikuwa miaka 20 iliyopita."kuhusu askari watoto.

Flash-Galerie Internationaler Tag gegen Einsatz von Kindersoldaten Red Hand Day
Mwanamuziki wa Bendi ya mitindo ya Rock BAP, Wolfgang Niedecken akiwa na Rais wa Ujerumani wa zamani Horst Köhler:Maadhimisho ya kupambana na matumizi ya watoto vitaniPicha: picture alliance/dpa

Askari watoto wa Uganda

Kwa hivyo, mwaka huo wa 2004 ambapo Uganda ilikuwa ikipigana vita vya wenyewe kwa wenyewe,Niedecken aliamua kuwashughulikia askari watoto.Wakati wa ziara hiyo Niedecken alikutana na wasichana wawili katika kituo kinachowasaidia askari watoto wa zamani kurejea katika maisha ya kawaida.  Watoto hao walitekwa nyara,walizuiliwa kama watumwa na walibakwa na waasi mara kwa mara. Baadae wasichana hao na watoto wao walipata Ukimwi. Yaliyowafika wasichana hao yalimhuzunisha sana na wakati huo akashindwa hata kuendelea na mahojiano yake na timu ya televisheni iliyofuatana nae katika ziara yake barani Afrika.

Flash-Galerie Internationaler Tag gegen Einsatz von Kindersoldaten Red Hand Day
Wema,Muziki na Haki za watoto:Mada zinazomgusa Wolfgang NiedeckenPicha: AP

Picha na Muziki

Niedecken si mwanamuziki tu bali ni mchoraji pia.Yeye amesomea uchoraji na picha zake zimewahi kuonyeshwa katika majumba ya sanaa nchini Ujerumani.Na muziki wake unajulikana kama ni wa midundo ya rock ya lahaja ya Kölsch yaani kutoka kanda ya Cologne.

Kwa njia fulani nyimbo zake zina ujumbe wa kisiasa na hata hisia za binafsi. Mwanamuziki Niedecken daima amepigania haki.Kwa mfano mwaka 1992,wageni waliposhambuliwa na wanazi mamboleo, Niedecken alitayarisha tamasha lililowaleta pamoja wanamuziki na mashabiki kuwapinga wafauasi wa sera kali za mrengo wa kulia.Sasa anashughulikia bara la Afrika. Anasema ameanzisha mradi maalum "Rebound" unaosaidia kuzijenga upya shule huko kaskazini ya Uganda.Kutakuwepo mabweni ili wanafunzi waweze kuishi huko wakati wa maosmo. Lengo ni kuwapa askari watoto wa zamani nafasi ya kujielimisha na kuanza maisha mapya. 

Kindersoldaten - Wolfgang Niedecken in Uganda
Wolfgang Niedecken, akiwa na wanafunzi wa Shule ya Muziki ya Kampala,UgandaPicha: picture-alliance/ dpa

Lakini hii leo,wageni mashuhuri na wasio mashuhuri watakapokutana mjini Bonn, Wolfgang Niedecken anataka kuwatumbuiza kwa muziki wake.

Mwandishi: Prema Martin-/ZPR-Görtz,Birgit

Mhariri: Othman,Miraji