1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Niger yavunja makubaliano ya kijeshi na Ufaransa

Mohammed Khelef
4 Agosti 2023

Utawala mpya wa kijeshi wa Niger umevunja mikataba yote ya kijeshi na Ufaransa, huku ukizuwia matangazo ya vyombo vya habari vya mkoloni wake huyo wa zamani, wakati muda wa mwisho uliowekwa na ECOWAS ukikaribia.

https://p.dw.com/p/4Ulzm
General Abdourahmane Tiani
Picha: REUTERS

Msemaji wa Umoja wa Ulaya, Nabila Massrali, aliandika kupitia mtandao wa X kwamba hatua ya utawala wa kijeshi wa Niger kuzuwia matangazo ya vyombo vya habari vya kimataifa vya Ufaransa ni "uvunjwaji wa wazi na mkubwa wa haki ya kutoa na kupata habari na pia uhuru wa kujieleza."

Vituo vya habari vya France24 na RFI vilisema matangazo yao yamefungiwa nchini Niger tangu jioni ya Alkhamis (Julai 3).

Soma zaidi: Utawala wa kijeshi waitisha maandamano makubwa Niger

Kauli ya Umoja wa Ulaya inakuja siku moja baada ya utawala wa kijeshi wa Niger kusema kuwa unakata makubaliano ya kijeshi na Ufaransa.

Tangazo hilo la usiku wa kuamkia Ijumaa kupitia televisheni ya taifa linazidisha mgawanyiko baina ya taifa hilo kubwa kwenye Jangwa la Sahara na mkoloni wake wa zamani, Ufaransa. 

Niger ilikuwa mshirika mkubwa wa Marekani kwenye kile kiitwacho vita dhidi ya ugaidi katika Ukanda wa Sahel.

Ujumbe wa ECOWAS waondoka patupu

Tangazo hilo pia limetoka zikiwa zimebakia siku mbili tu kabla ya muda wa mwisho uliowekwa na Jumuiya ya Uchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) kwa utawala wa kijeshi kumuachia huru na kumrejesha madarakani Rais Mohamed Bazoum ama ukabiliwe na uwezekano wa kutumiwa nguvu.

Nigeria Abuja | ECOWAS-Treffen zur Lage in Niger
Viongozi wa majeshi ya mataifa ya Jumuiya ya Uchumi wa Afrika Magharibi (ECOWAS) waliokutana mjini Abuja, Nigeria, kujadili hatua za kuichukulia Niger.Picha: KOLA SULAIMON/AFP

Mwenyewe Bazoum amechapisha makala kwenye gazeti la Washington Post akisema "Naandika kama mateka" na akaiomba Marekani na washirika wake waiokowe nchi yake.

Soma zaidi: Viongozi wa kijeshi wa Niger kujibu jaribio lolote la kichokozi

Ujumbe uliotumwa na ECOWAS kuzungumza na utawala huo ulilazimika kuondoka jioni ya jana bila kukutana na kiongozi wa kijeshi, Jenerali Abdourahmane Tchiani, wala hata kuwasili kwenye mji mkuu, Niamey. 

Mabalozi wafutwa kazi

Utawala huo tayari umewafuta kazi baadhi ya mabalozi waliokuwa wakihudumu chini ya serikali iliyopinduliwa. 

Pro-Putsch-Demo in Nigers Hauptstadt Niamey
Maandamano ya maelfu ya raia wa Niger wakiunga mkono jeshi la nchi hiyo na kumlaani mkoloni wa zamani, Ufaransa.Picha: AFP/Getty Images

Miongoni mwa waliofukuzwa kazi ni mabalozi waliokuwa wakiiwakilisha Niger nchini Marekani, Ufaransa, Togo na Nigeria, ambayo ndiyo inayoongoza jumuiya ya ECOWAS.

Soma zaidi: Kitisho cha baadhi ya majirani wa Niger kwa ECOWAS ni onyo kwa Afrika

Wakati huo huo, umewataka wananchi wa taifa hilo la Afrika Magharibi kuwa na hadhari na majeshi na majasusi ya kigeni na kuapa kuchukuwa hatua kali dhidi ya yeyote atakayejaribu kuingilia mambo yake ya ndani.

"Uchokozi wowote ama jaribio la uchokozi dhidi ya taifa la Niger litakabiliwa na jibu la haraka bila kutolewa onyo."  Alisema msemaji wa utawala wa kijeshi, Kanali Meja Amadou Abdramane.

Mali, Burkina Faso na Guinea, ambazo pia zinaongozwa na tawala za kijeshi, zimetangaza wazi kuwa endapo Niger itavamiwa kijeshi, nazo zitachukulia uvamizi huo kuwa ni dhidi yao.

Vyanzo: AFP,AP