1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria: Kundi la Boko Haram lawaua watu 69

Saleh Mwanamilongo
10 Juni 2020

Watu 69 wameuwawa na wanamgambo wa Bokoharam kaskazini mashariki mwa Nigeria. Shambulizi hilo linadaiwa kuwa ni la ulipizaji kisasi.

https://p.dw.com/p/3dbKb
Nigeria Islmischer Staat in West Afrika ISWAP Truck
Picha: Getty Images/AFP/A. Marte

Viongozi wa nchi hiyo wanasema kwamba shambulio la wanamgambo hao lilifanyika siku ya Jumanne kwenye kijiji cha Foduma Kolamaiya, kwenye mkoa wa Gubio, jimbo la Borno. Wakaazi wa eneo hilo wanaelezea kuwa shambulizi hilo ni ulipizaji kisasi dhidi ya raia ambao walipinga kuvamiwa kwa kijiji chao wiki kadhaa zilizopita.

"Walikuja kwa pikipiki na gari na waliuwa watu kadiri walivyotaka katika shambulio lililodumu masaa mawili" Amesema Rabiu Isa, mmoja wa wanachama wa kundi la ulinzi wa umma kwenye eneo akiongeza kuwa walihesabu maiti 69 na kuthibitisha kwamba huenda idadi ikaongezeka kwa sababu kuna wengine waliotoeka na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Malam Bunu, mmoja wa viongozi wa kundi la ulinzi wa umma kwenye eneo hilo amesema wanamgambo hao walirejea Jumatano asubuhi na kumuuwa mfugaji mmoja na baadae kuchoma moto kijiji hicho kabla ya kuondoka.

Bunu ameliambia shirika la habari la AP kwamba moto uliendelea kuwaka kwenye kijiji hicho cha mkoa wa Gubio, umbali wa kilomita 100 kaskazini magharibi mwa mji wa Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la Borno. Wengi miongoni mwa wakaazi wa jimbo hilo ni wafugaji ambao kwa miaka kadhaa wamejihami kufuatia mashambulizi ya wanamgambo wa Boko Haram.

Wanajeshi wa Nigeria wakifanya doria kusini mashariki mwa nchi hiyo. (Picha ya maktaba)
Wanajeshi wa Nigeria wakifanya doria kusini mashariki mwa nchi hiyo. (Picha ya maktaba)Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Bunu amesema baada ya mashambulizi ya Jumanne, ngombe 1,200 waliibwa. Vikosi vya usalama vilitumia ndege ya jeshi la Nigeria kuwafyatulia wanamgambo hao risasi walipokuwa wakitoroka.

Boko Haram lalipiza kisasi?

Shambulizi la Jummanne ni ulipizaji kisasi baada ya raia kuwauwa wanamgambo wawili wa Bokoharam walipojaribu kukishambulia kijiji chao miezi miwili iliyopita.

Mara nyingi wanamgambo hao wa Boko Haram hushikilia mifugo ya raia ili kuwalazimisha kulipa ushuru usio halali, lakini raia hao wameanza kukaidi masharti hayo, alisema Bunu.

Kundi la Boko Haram linalojihusisha na mambo ya kigaidi, limedumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa na limeuwa maelfu ya watu na makumi ya maelfu wengine kulazimika kuyahama makaazi yao.

Hivi karibuni wanamgambo hao waliweka vizuwizi vya barabarani ili kuwazuia wasafiri na kuwateka nyara  kaskazini mwa jimbo la Borno. Hayo yamesemwa na Ahmed Shehu ambaye kiongozi wa mashirika ya kiraia ya jimbo hilo.

Watu watano akiwemo kiongozi wa huduma za dharura wa jimbo la Borno, walitekwa nyara. Jumapili, wafanyakazi wa umma na waalimu walitekwa nyara na baadae kuachiwa huru.

Chanzo: APE