1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yajiandaa kuamua

27 Machi 2015

Kampeni za kuwania kiti cha urais nchini Nigeria zimemalizika rasmi usiku wa Alhamisi, ambapo rais wa sasa Goodluck Jonathan anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kiongozi wa zamani wa kijeshi Muhammadu Buhari.

https://p.dw.com/p/1EyLV
Wagombea wakuu Rais goodluck Jonathan na mpinzani wake Muhammadu Buhari
Wagombea wakuu Rais goodluck Jonathan na mpinzani wake Muhammadu BuhariPicha: DW/Ubale Musa

Mipaka ya nchi kavu na ya baharini ilifungwa usiku wa Jumatano kama sehemu ya hatua thabiti za kiusalama ambazo pia zinahusisha marufuku ya masaa manane ya kutembeatembea wakati vituo vy akupigia kura vitakapofunguliwa siku ya Jumamosi.

Nigeria ina historia ya ghasia zinazotokana na uchaguzi, na wagombea hao wawili walionekana kuwa makini kuzuwia marudio ya matukio ya mwaka 2011, ambapo watu 1,000 waliuawa katika makabiliano yaliyofuatia kutangazwa kwa matokeo.

Mkuu wa tume ya uchaguzi ya Nigeria INEC Attahiru Jega.
Mkuu wa tume ya uchaguzi ya Nigeria INEC Attahiru Jega.Picha: Stringer/AFP/Getty Images

Amani na utulivu ni nguzo kuu

Jonathan na Buhari walisaini waraka wa kuepuka vurugu mwezi Januari na jana Alhamisi walirejea dhamira yao juu ya uchaguzi huru, na kutoa wito kwa raia na wafuasi wa vyama vyao kujiepusha na vurugu au vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga maono yao ya pamoja ya kuwa na uchaguzi huru na unaokubalika.

Rais Jonathan alichapisha ujumbe wa ahasante kwa Wanigeria kwenye kurasaza mbele za magazeti kadhaa ya kitaifa, yakiwa na toleo maalumu la kurasa 40 linalobainisha yale anayodai kuyatimiza.

Lakini rais huyo pia alitambua changamoto kutoka kwa Buhari na chama chake cha All Progressive Congress APC, ambacho kinaweza kukishinda chama chake tawala kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi mwaka 1999.

Jonathan ameendesha kampeni ya mwendelezo, na ameapa kukamilisha kazi aliyoianzisha wakati wa kipindi chake cha miaka minne madarakani.

APC yapania mabadiliko

Kwa upande wake, Buhari mwenye umri wa miaka 72, ambaye aliongoza serikali ya kijeshi katika miaka ya 1980, ameendesha kampeni ya mabadiliko.

Amekosoa ukosefu wa usalama, kuvunjika kwa miundombinu na pengo linaloongezeka kati ya walicho nacho na wasio nacho, akiapa kuchukuwa hatua dhidi ya Boko Haram na kupambana na rushwa.

"Uchaguzi wa rais Jumamosi hii unatoa fursa ya kipekee kwa Wanigeria kujitokeza kwa wingi na kupiga kura kuiondosha serikali dhaifu madarakani," alisema Buhari wakati akihitimisha kampeni yake.

Kundi la Boko Haram limekuwa Agenda muhimu ya kampeni za uchaguzi huu.
Kundi la Boko Haram limekuwa Agenda muhimu ya kampeni za uchaguzi huu.Picha: picture alliance/AP Photo

Tume ya uchaguzi yasema iko tayari

Tume yenye dhima ya kuandaa uchaguzi huo katika taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika, ilisema iko njiani kuendesha zoezi hilo kwa amani. Karibu wapigakura milioni 68.8 kati ya jumla ya raia milioni 173 wamejiandikisha kupiga kura nchini Nigeria, ambayo pia ndiyo nchi inayoongoza kwa uchumi mkubwa barani Afrika.

Karatasi za kura na vifaa vingine vya uchaguzi, vikiwemo kwa mara ya kwanza vifaa vya kisasa vya mkononi vya kuhakiki vitambulisho vya wapigakura, vimetumwa katika majimbo 36 ya Nigeria na eneo la mji mkuu.

Msemaji wa tume ya uchaguzi Kayode Idowu alisema uchaguzi huo hautakuwa na udanganyifu na kwamba matokeo yatatangazwa ndani ya masaa 48 baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura siku ya Jumamosi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,ape
Mhariri: Josephat Nyiro Charo