1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
HistoriaAfrika

Oba Ewuare: Mfalme wa shaba wa mji wa Benin

Yusra Buwayhid
11 Julai 2021

Oba Ewuare bado anakumbukwa kwa kuupanua ufalme wa Benin, kuendeleza sanaa na kuimarisha uchongaji wa vichwa vya shaba ambavyo hii leo ni maarufu kote ulimenguni.

https://p.dw.com/p/3n7un
Asili ya Afrika | Oba Ewuare
Oba Ewuare

Oba Ewuare: Mfalme aliyeleta shaba mji wa Benin

Oba Ewuare aliishi nyakati zipi?

Oba Ewuare ambaye pia anajulikana kama Oba Ewuare I ama Ewuare Mkuu, alitawala kama mfalme wakati wa Ufalme wa Benin kuanzia 1440 hadi 1473. Alikuja kuwa Oba wa Benin baada ya kumpindua ndugu yake wa kiume Uwaifiokun. Mapinduzi hayo ya vurugu uliugeuza Mji wa Benin kuwa magofu. Lakini baadae alifanikiwa kuujenga tena, hadi ukaja kujulikana kama himaya kubwa na maarufu Afrika Magharibi.

Utawala wa Oba Ewuare ulikuwa wa aina gani?

Wakati wa utawala wa Ewuare, mji mkuu wa Benin ulikuwa umepangika vizuri kuweza kuhudumia idadi kubwa ya wakazi wake. Inasemekana alijenga milango tisa tofauti ya kuingilia Benin na kusimamia ujenzi wa barabara kadhaa. Utamaduni wa fasihi simulizi unamuelezea mfalme huyo kama mchawi mwenye busara, tabibu na shujaa.

African Roots | Oba Ewuare 3
Asili ya Afrika

Oba Ewuare wa Benin anafahamika kwa sanaa gani?

Upanuzi wa sanaa ya Benin umebakia kuwa moja ya vitu vikuu anavyokumbukiwa Oba Ewuare. Aliwaalika wataalamu wa kazi za mikono jijini Benin na kuhimiza utengenezaji wa vitu vya sanaa vyenye ubora. Halikadhalika, alianzisha utamaduni wa kuchonga vichwa vya shaba kama namna ya kuwakumbuka kwa heshima wafalme wa Benin waliotangulia. Kazi hizo za sanaa zimehifadhiwa katika makumbusho tofauti haswa  Nigeria lakini pia kote ulimwenguni. Juhudi za Ewuare za kukuza sanaa zilipelekea kuanzishwa kwa tasnia ya sanaa iliyokuwa ikizingatia zaidi kutengeneza mapambo ya pembe za ndovu, mbao, shaba ambayo yapo hadi hivi sasa.

African Roots | Oba Ewuare 6
Asili ya Afrika

Kwa namna gani utamaduni ulinawiri chini ya utawala wa Oba Ewuare?

Oba Ewuare pia anajulikana kwa kukuza shughuli za kitamaduni za Benin. Alianzisha tamasha la Igue ambalo hadi hii leo ni hafla muhimu kwa watu wa Benin.Pia, Oba Ewuare alianzisha matumizi ya shanga za matumbawe zenye kupendeza, ambazo hadi hii leo zinatumika kama mampambo ya kifalme na katika mavazi ya kitamaduni ya Benin. Leo, sio tu Benin inayotumia shanga za matumbawe, bali mapambo hayo yameenea katika sehemu kadhaa za Kusini mwa Nigeria.

Je, kuna mafanikio gani mengine ya Oba Ewuare?

African Roots | Oba Ewuare 7
Asili ya Afrika

Mara nyingi Ewuare anajulikana kama Oba wa kwanza wa Benin sio kwa sababu alikuwa wa kwanza kutawala Ufalme wa Benin lakini kwa sababu alikuwa Oba wa kwanza kuleta mabadiliko makubwa.Alirithi ufalme mdogo lakini alifanikiwa kuupanua na kujumuisha ndani yake miji na vijiji kadhaa. Aidha hatua kadhaa za kiutawala alizozianzisha zilirahissiha suala la kukabidhiana utawala, na likawa linafanyika kwa amani hadi hii leo. Hivyo Ufalme ukawa unarithiwa na mtoto wa kwanza wa kiume, na kumaliza mivutano inayojitokeza ya kila pale anapokufa mfalme.

Asili ya Afrika: Oba Ewuare

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.