1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

240708 berlin obama

Charo, Josephat24 Julai 2008

Seneta Barack Obama anatarajiwa kutoa hotuba ya kihistoria mjini Berlin leo jioni.

https://p.dw.com/p/EjA4
Seneta Barack Obama (kushoto) akisalimiana na kansela Angela Merkel mjini BerlinPicha: AP

Akiwa katika kituo chake cha kwanza cha ziara yake barani Ulaya Barack Obama amefanya mazungumzo na kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa muda wa saa moja. Viongozi hao wamezungumza kuhusu mgogoro wa nyuklia wa Iran, Afghanistan, Pakistan na mchakato wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Ujerumani, Ulrich Wilhelm, mazungumzo hayo yamekuwa mazuri na ya kina na yamefanyika kwa njia ya uwazi. Barack Obama na kansela Merkel wamejadiliana pia kuhusu sera za kibiashara na mazingira lakini sana juu ya uhusiano kati ya Marekani na bara la Ulaya na maswala ya sera za nje. Kwa kutimia ziara yake barani Ulaya na hususan hotuba atakayoitoa leo jioni katika mnara wa ushindi wa Siegessäeule mjini Berlin kuimarisha sera yake ya kigeni.

Uzoefu

John Kornblum, aliyekuwa balozi wa Marekani mjini Berlin wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, anasema mkakati huo wa Obama unafaa kabisa.

´´Obama hana uzoefu mkubwa katika maswala ya siasa za kigeni na anajaribu hivi sasa kujipatia uzoefu huo kutumia ziara hii. Jambo la pili ni kwamba sifa ya Marekani katika nchi za nje imeharibika sana. Na naweza kumwambia kile ambacho kimeripotiwa na vyombo vya habari nchini Marekani, pongezi nyingi kwa kufanya ziara za kufana nchini Afghanistan na Irak. Nadhani anatumia ziara hii kudhihirisha umahiri wake, lakini pia kuwadhihirishia Wamarekani vipi anavyoweza kuiimarisha tena sifa ya Marekani ulimwenguni.´´

Kisa

Kabla kutoa hotuba yake hii leo Barack Obama atakutana na meya wa mji wa Berlin Klaus Wowereit wa chama cha Social Democratic, SPD na waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier ambaye pia ni wa chama hicho cha SPD. Mwendo wa saa moja leo jioni, Obama atahotubia umari wa wati takriban laki moja kwa dakika 45.

Hata hivyo maandalizi ya hotuba hiyo yametatizwa wakati mwanamume mmoja alipovuka utepe wa polisi unaozunguka eneo ililofungwa akiwa ndani ya gari lake na kumwaga rangi nyekundu katika eneo atakapohutubia seneta Obama. Mwanamume huyo kutoka jimbo la Baden Wuerttemberg sasa anazuiliwa na polisi akisubiri uchunguzi.

Ushabiki

Huku mji wa Berlin ukiwa umegubikwa na homa ya Obama, wachambuzi wa kisiasa wamesisitiza kwamba ziara yake inalenga kumuongezea nafasi ya kushinda kinyang´anyiro cha kuwania urais wa Marekani mwezi Novemba mwaka huu.

Katika hotuba yake Obama anatarajiwa kuufufua uhusiano kati ya Marekani na Ulaya ambao umezorota kwa kiasi fulani wakati wa utawala wa rais George W Bush. Watu wanasubiri kusikia ikiwa Obama atazitaka nchi za Ulaya kuongeza idadi ya wanajeshi nchini Afghanistan na msimamo wake kuhusu kuishinikiza Iran iachane na mpango wake wa kurutubisha madini ya uranium.