1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ataka waumini kuvumiliana.

Halima Nyanza11 Septemba 2010

Wakati leo ikitimia miaka tisa tangu kutokea kwa shambulio la kigaidi mjini New York, Septemba 11 2001, Rais Barack Obama wa Marekani ametoa wito wa kuwepo kuvumiliana kwa waumini wa dini tofauti.

https://p.dw.com/p/P9fG
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: AP

Ameyasema hayo jana, katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Washington, Rais Barack Obama amesema pia kwamba nchi yake haiwezi kugawanyika kwa misingi ya dini.

Rais Obama ametoa kauli hiyo jana, wakati nchi yake ikiwa katika wakati mgumu, kufuatia mipango iliyotangazwa awali na kasisi wa kanisa moja nchini Marekani Tery Jones ya kutishia kuchoma moto nakala za kitabu kitukufu cha waislamu, Koran leo, kama kuadhimisha kumbukumbu ya miaka tisa tangu kutokea shambulio la kigaidi la Septemba 11, mwaka 2001..

Dossierbild Koran-Verbrennung 1
Kasisi Terry Jones, asitisha mipango yake ya kuchoma nakala za Koran.Picha: AP

Aidha rais Obama alifafanua pia kwamba hawako katika vita na Uislamu ila wako katika vita na makundi ya kigaidi, ambayo yamepotosha  uislamu ama kutumia dini hiyo kufanya maovu yao.

Na katika kile kilichoonekana kugusia mipango ya ujenzi wa msikiti karibu na eneo llilipotokea shambulio la Septemba 11, Rais Obama alisema waislamu pia wana haki ya kujenga popote na kwamba Marekani inatoa uhuru sawa kwa watu wote wanawake kwa wanaume na haki yao ya kuabudu.

Reaktionen zu Terry Jones' Koran-Plänen
Wananchi wa Afghanistan wakiandamana kupinga mipango ya kasisi Terry Jones.Picha: AP

Serikali ya Marekani imekuwa na wasiwasi kuwa mpango huo wa kuchoma moto nakala za Koran utahatarisha maisha ya wanajeshi wao, wanaohudumu nchini Afghanistan na Iraq.

Katika hatua nyingine, Imam Feisal Abdul Rauf ambaye anaongoza juhudi za ujenzi wa msikiti katika eneo lililokaribu na kilipokuwa kituo cha biashara kilichoteketezwa katika shambulio la bomu la Septemba 11, mwaka 2001 nchini Marekani, amesema hana mipango yoyote ya kukutana na kasisi Terry Jones ambaye ametishia kuchoma moto nakala za kitabu kitukufu cha waislamu,Koran.

Imam Feisal Abdul Rauf
Imam Feisal Abdul Rauf.Picha: ap

Awali Kasisi huyo pamoja na wafuasi wake, kwa siku kadhaa walipanga kuchoma moto nakala za koran, kwa kile alichodai kuadhimisha kumbukumbu hiyo ya leo.

Kasisi huyo amekubali kuachana na mipango yake hiyo, na kutaka kukutana na Imam Rauf ambaye amedai kuwa amekubali kuhamisha ujenzi katika eneo hilo na kwamba wao wamekubali kufuta mpango wao wa kuchoma moto nakala za Koran leo.

11. September Gedenken 2009 Flash-Galerie
Watu wakiangalia ujenzi unavyoendelea katika eneo lililokuwa na kituo cha biashara cha kimataifa kilichoteketezwa katika shambulio la Septemba 11, mwaka 2001.Picha: AP

Hata hivyo Imam Feisal Abdul Rauf, ambaye anaongoza ujenzi wa msikiti huo alikanusha taaraifa hizo, kwa kusema kuwa hajawahi kuwasiliana na kasisi huyo.