1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama, Romney katika ngwe ya lala salama

2 Novemba 2012

Wagombea wa kiti cha urais nchini Marekani wameanza ngwe ya lala salama, wakijaribu kuwashawishi wafuasi wao na wale ambao hawajafanya uamuzi wa nani wamchague katika kura ya Jumanne ijayo.

https://p.dw.com/p/16bki
Obama na Romney wakisalimiana na wafuasi wao baada ya moja wa mijadala ya wazi.
Obama na Romney wakisalimiana na wafuasi wao baada ya moja wa mijadala ya wazi.Picha: AP

Rais Barack Obama na mpinzani wake wa chama cha Republican Mitt Romney walisitisha kampeni zao kwa muda kufuatia tufani iliyosababishwa na kimbunga cha Sandy, kilichoikumba pwani ya mashariki. Obama alirejea katika kampeni siku ya Alhamis kwa mikutano ya mfululizo katika majimbo ya Wisconsin, Nevada na Colrado, wakati mpinzani wake alifanya kampeni katika jimbo la Virginia. Wote watakuwa katika jimbo muhimu la Ohio leo Ijumaa.

Rais Obama akimkumbatia mwathirika wa kimbunga cha Sandy, wakati akizuru jimbo la New Jersey kujionea uharibifu uliyofanywa na kimbunga hicho.
Rais Obama akimkumbatia mwathirika wa kimbunga cha Sandy, wakati akizuru jimbo la New Jersey kujionea uharibifu uliyofanywa na kimbunga hicho.Picha: Reuters

Akizungumza na umati mjini Las Vegas, Nevada, Obama aliwamuagia sifa raia wa Marekani kwa kuungana pamoja katika wakati mgumu wa maafa yaliyosababishwa na kimbunga cha Sandy, na kuwaomba wamuongeze miaka mingine minne ofisini. Obama alimshambulia mpinzani wake kwa kile alichosema ni kutaka kudandia kaulimbiu yake ya mabadiliko.

"Sasa katika wiki hizi za lala salama za kampeni hii, gavana Romney amekuwa akitumia ujuzi wake kama afisa mauzo kupamba sera zile zile zilizouangusha uchumi wetu--sera zile zile ambazo tumekuwa tukipambana kuondoa madhara yake kwa miaka minne iliyopita---na sasa anazipendekeza kama njia ya mabadiliko," alisema Obama. Aliongeza kuwa anachokipendekeza Romney siyo mabadiliko ya uhakika --kuyaongezea nguvu mabenki siyo mabadiliko -- na pia kuwaacha mamilion bila bima ya afya nayo siyo mabadiliko.

Gavana Mitt Romney akibeba chupa za maji kuzipakia kwenye gari wakati akishiriki kampeni ya kukusanya misaada kwa ajili ya wathirka wa kimbunga Sandy.
Gavana Mitt Romney akibeba chupa za maji kuzipakia kwenye gari wakati akishiriki kampeni ya kukusanya misaada kwa ajili ya wathirka wa kimbunga Sandy.Picha: dapd

Akipambana kuepuka kuachwa nyuma baada ya Obama kung'ara kufuatia namna alivyoushughulikia mgogoro wa kimbunga cha Sandy, Romney alihutubia mikutano mitatu katika jimbo la Virginia, ambako alijaribu kuirudisha kampeni kwa hoja yake ya uchumi mbaya. "Kwa kweli hatuwezi kuwa na miaka mingine minne kama miaka minne iliyopita. najua kambi ya Obama wanaimba miaka minne mingine lakini wimbo wetu ni huu--siku tano nyingine----"

Meya wa New York, Jarida la The Economist wamuunga mkono Obama

Kampeni ya Obama ilipata msukumo siku ya Alhamis baada ya Meya wa jiji la New York Michael Bloomberg kutangaza kumuunga mkono kwa miaka minne zaidi, akisifia namna rais huyo alivyoshughulikia tufani ya Sandy na kubainisha kuwa Obama ndiye aliye na uwezo wa kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Alisema wakati Romney alichukua hatua za kukabiliana na tabianchi akiwa gavana wa jimbo la Massachusetts, amekuwa anabadilisha misimamo yake mara kwa mara. Bloomberg alikuwa mwanchama wa chama cha Republican lakini sasa analiongoza jiji hilo kubwa duniani bila kupitia chama chochote.

Jarida linaloheshimika sana la The Economist lenye makao yake London, Uingereza nalo lilitangaza siku ya Alhamis kwamba linamuunga mkono rais Barack Obama kwa awamu ya pili, ingawa si kwa ari kama ile ya miaka minne iliyopita. Jarida hilo lilisema katika habari yake kuu kuwa wakati Marekani inakabiliwa na uamuzi mgumu na kampeni chafu zaidi ya mwaka 2008, mpiznani wa Obama hastahiki kuwa rais wa Marekani.

Meya wa jiji la New York Michael Bloomberg ametangaza kumuunga mkono rais Barack Obama kwa awamu ya pili.
Meya wa jiji la New York Michael Bloomberg ametangaza kumuunga mkono rais Barack Obama kwa awamu ya pili.Picha: Reuters

Kwa upande mwingine, raia wengi wa Israel wanaombea Mitt Romney ashinde kinyanganyiro hicho kwa sababu wanamuona kama rafiki bora wa taifa hilo la kiyahudi kuliko rais Obama. Lakini wapalestina wao wanaona hakutana tofauti kati ya wagombea wote.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, dpae,
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman