1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ziarani nchini China

Sekione Kitojo17 Novemba 2009

Rais wa Marekani Barack Obama na mwenyeji wake rais wa China Hu Jintao wamekubaliana juu ya kuimarisha uhusiano wao zaidi katika masuala ya uchumi, mabadiliko ya hali ya hewa na nishati.

https://p.dw.com/p/KZEn
Rais wa Marekani Barack Obama akihutubia katika ziara yake nchini China.Picha: AP

Rais wa Marekani Barack Obama na mwenyeji wake rais wa China Hu Jintao wamekubaliana juu ya kuimarisha uhusiano wao zaidi katika masuala ya uchumi,mabadiliko ya hali ya hewa,nishati na vitisho vya kinuklia kutoka nchi za Iran na Korea Kaskazini. China na Marekani zimeahidiana leo kuimarisha mabadishano ya mambo ya kijeshi na kulinda matumizi ya amani ya anga za juu baada ya mazungumzo ya viongozi hao wawili. Hata hivyo viongozi hao wawili wameonekana bado wanatofautina katika masuala ya uchumi,usalama na haki za binadamu,masuala ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakiutatiza uhusiano wa mataifa hayo mawili yenye nguvu. Obama ni rais wa kwanza wa Marekani kuitembelea China katika kipindi cha miaka 12.

Viongozi hao wawili wameahidi kuchukua hatua muhimu kuendeleza uhusiano endelevu wa kijeshi katika siku za usoni kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano wao katika mji mkuu wa China Beijing.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa pande zote mbili zinajitayarisha na ziara za maafisa wao wa ngazi ya juu , ikiwa ni pamoja na Jenerali Chen Bingde mkuu wa jopo la majenerali wa jeshi la China, na waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates.

Taarifa hiyo hata hivyo haikutoa muda maalum wa ziara hizo.

Wasi wasi wa kijeshi kati ya nchi hizo umejitokeza hivi karibuni, ukichochewa na ongezeko la majeshi ya China pamoja na makabiliano kadha baharini . Pande zote zitatekeleza mabadilishano ya kijeshi pamoja na mpango wa ushirikiano ambao utaongeza kiwango na mabadilishano ya mara kwa mara, taarifa hiyo imesema.

Lengo la juhudi hizi ni kuimarisha uwezo wao kwa ajili ya ushirikiano bora zaidi na kuweza kuwa na maelewano makubwa zaidi ya nia ya kila upande pamoja na mazingira ya kiusalama duniani.

China na Marekani pia zimekubaliana kuwa Iran ni lazima ionyeshe mpango wake wa kinuklia ni kwa ajili ya matumizi ya amani, na uwazi, rais Barack Obama amesema leo , lakini rais Hu Jintao wa China alichukua tahadhari zaidi kuhusu mzozo huo.

Rais Obama amesema kwamba serikali ya mjini Tehran itachukuliwa hatua zinazostahili ikiwa haitothibitisha kwamba mpango wake wa kinuklia ni kwa ajili ya matumizi ya amani na kuwa wazi kuhusu mpango huo.Obama amesema Marekani na China zitashirikiana kukikabili kitisho cha Iran ikiwa itamiliki silaha za kinuklia.Pia amesema baraza la usalama la Umoja wa mataifa linazungumza kwa kauli moja dhidi ya mpango huo wa Iran.

Kwa upande wake rais Hu Jintao wa China amezungumzia zaidi juu ya diplomasia katika suala hilo la Iran ili kuimarisha usalama katika eneo la mashariki ya kati. Kuhusu Korea Kaskazini nchi zote mbili zinataka mazungumzo ya pande sita yaanze haraka iwezekanavyo.Akizungumzia hilo rais wa China alisema-

''Tumefikiana kwa pamoja kubakia katika lengo la kuutatua mzozo wa nuklia wa Korea kaskazini kupitia mazungumzo,na hatua hiyo itatuwezesha sote tunaohusika katika suala hilo kufikia lengo letu.Pande zote mbili zitafanya kazi pamoja na wahusika wengine kuendelea na mpango wa kuishawishi Korea kaskazini kuachana na harakati zake na kurudi kwenye mazungumzo ya pande sita ili kuimarisha amani na usalama katika eneo la kaskazini mashariki mwa Asia''

Suala jingine muhimu lililojadiliwa na viongozi hao ni kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa rais Obama amesema

lengo la pande hizo mbili katika mkutano wa Copenhagen sio kupata makubaliano ya kupendelea upande fulani au azimio la kisiasa bali wana nia ya kufikia makubaliano yatakayojumuisha masuala yote na ambayo yatatekelezwa.

''Nchi zetu kama watumiaji wakubwa na watoaji wa nishati hakuwezi kupatikana suluhisho katika changamoto hii bila ya juhudi zetu na ndio sababu tumekubaliana juu ya mipango kadhaa ikiwa ni pamoja na kuunda kituo cha utafiti wa nishati na kuafikiana kuhusu matumizi ya nishati isiyoharibu mazingira na pia kushirikiana kufikia mafanikio katika mkutano wa Copenhagen''

Ama kuhusu suala la Uchumi rais Obama ameitaka China kushirikiana na Marekani katika kuuongoza ulimwengu kujikwamua kutokana na mgogoro wa kiuchumi unaoendelea lakini juu ya hilo pia wamekubaliana kufuatilia ahadi zilizotolewa katika mkutano wa G20 mjini Pittsburg na kutafuta mkakati wa kuimarisha uchumi.

Hata hivyo rais wa China ameitaka Marekani kuacha mtindo wa kujipendelea katika kuhami masoko, pamoja na kukataa kuitambua China kama soko kamili la kiuchumi na kudhibiti biashara ya technologia ya juu.

Na hatimae katika suala la haki za binadamu rais Obama alionekana kuchokoza nyuki aliposema kwamba makundi ya waliowachache nchini China yanabidi kupewa haki zao kibinadamu zinazostahili na kuitolea mwito nchi hiyo kurudi katika meza ya mazungumzo na wajumbe wa kiongozi wa kidini wa Tibet Dalai Lama anayeishi uhamishoni. Matamshi hayo yalijibiwa kwa sauti kali na rais Hu Jintao akisema pande zote mbili zimehakikishiana juu ya msingi wa kuheshimiana na kuheshimu uhuru wa mamlaka ya kila upande Kutokana na hilo China itaendelea kuchukua hatua ya kudumisha usawa,kuheshimiana,na kutoingilia kati masuala ya ndani ya upande wa pili.

Mwandishi Sekione Kitojo / DPAE/RTRE/AP

Mhariri:Abdul-Rahman