1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OCHA: Watu 25 waliuliwa Malakal

Admin.WagnerD4 Machi 2016

Umoja wa Mataifa umesema watu wapatao 25 waliuawa na wengine 120 kujeruhiwa wakati watu waliokuwa na bunduki waliovalia sare za jeshi walipoishambulia kambi ya umoja huo Sudan Kusini mwezi uliopita.

https://p.dw.com/p/1I7LV
Südsudan UN-Schutz Flüchtlinge in Malakal
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Kauli ya Umoja wa Mataifa inakuja wiki mbili baada ya makabiliano makali ya risasi katika kambi hiyo iliyokuwa ikitumika kama makazi ya raia katika mji wa Malakal, kaskazini mashariki mwa Sudan Kusini. Ripoti iliyotolewa leo na afisi ya Umoja wa Mataifa, inayoratibu misaada, OCHA, imeeleza kwa kina kushindwa kwa wanajeshi wa kulinda amani kuwalinda raia waliokuwa wamekimbilia hifadhi katika kambi hiyo.

Zaidi ya raia 47,000 walikuwa wakiishi katika kambi hiyo baada ya kukimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka Desemba 2013. Umoja wa Mataifa umesema shambulizi hilo huenda ni uhalifu wa kivita. OCHA imesema makazi ya familia 3,700 yaliharibiwa kwa kuchomwa moto wakati wa mapigano, pamoja na vituo vya kutoa huduma za kibinaadamu zikiwemo zahanati, matangi ya kuhifadhia maji, vituo vya utoaji chakula na shule.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Farhan Haq, naibu wa msemaji wa katibu mkuu wa umoja huo, alisema, "Panahitajika kuwepo uratibu wa masuala ya kibinaadamu. Washirika wetu wamepeleka maafisa zaidi pamoja na misaada kukidhi mahitaji mapya huko Malakal na jimbo la Upper Nile. Chakula kimegawiwa watu zaidi ya 40,000, huku zaidi ya watoto 8,600 wakipewa chakula cha ziada."

Südsudan Verletzter in Malakal
Mwanamume aliyejeruhiwa na kukimbia mapigano Malakal akiwa hospitali ya JubaPicha: picture-alliance/dpa

Wakazi wa mji wa Malakal wanasema watu 46 waliuliwa katika shambulizi la Februari 17-18, lakini Umoja wa Mataifa umeitangaza idadi hiyo kuwa 25, badala ya 18 iliyoripotiwa awali.

Miongoni mwa waliouawa ni wafanyakazi watatu wa mashirika ya misaada, wawili kati yao wafanyakazi wa huduma za afya wa Sudan Kusini waliofanya kazi na shirika la madaktari wasio na mipaka, MSF. Shirika hilo lililowatibu watu 46 waliokuwa na majeraha ya risasi, limesema mmoja wa wafanyakazi hao aliuawa alipokuwa akitoa huduma na watu wengine waliojaribu kuuzima moto au kuwasaidia majeruhi walilengwa makusudi na kupigwa risasi.

Watu walichomwa wakiwa hai

Wakazi wanasema baadhi yao walichomwa hadi kufa katika moto ulioanzishwa kwa makusudi ulioyaharibu baadhi ya maeneo ya kambi hiyo ya kijeshi, ambako raia waliishi katika makundi kulingana na kabila ili kupunguza machafuko ya kikabila.

Shirika la madakari wasio na mipaka limesema kutokana na shambulizi hilo raia wengi waliokuwa wakiishi katika kambi hiyo sasa hawana chochote. Alipoulizwa ni watu wangapi waliouliwa, msemaji wa tume ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani, Herve Ladsous, alisema Jumatano wiki hii kwamba wameshindwa kuhesabu.

Tangu shambulizi la Malakal mapigano katika mji mdogo wa Pibor mashariki mwa Sudan Kusini mnamo Februari 21 yaliwalazimu maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao wakati watu waliojihami na bunduki walipozivamia kambi za mashirika matano ya misaada, ikiwemo zahanati ya shirika la madakatari wasio na mipaka, na kuiba.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe

Mhariri:Mtullya Abdu