1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Omar al Bashir ahamishwa katika jela la Kobar

Amina Mjahid
17 Aprili 2019

Viongozi wa kijeshi wa Sudan wamemhamishia rais aliyepinduliwa Omar al-Bashir katika jela ya Khobar ya mji mkuu Khartoum. Duru za kuaminika zinasema anashikiliwa peke yake na katika ulinzi mkali.

https://p.dw.com/p/3GzBC
Sudan Weiterhin Proteste |
Picha: Reuters/M. Nureldin Abdallah

Al-Bashir amehamishiwa jela huku mamia ya wasudan wakiendelea kupiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum wakitoa wito madaraka wakabidhiwe haraka raia.

"Tangu alipong'olewa madarakani alkhamisi iliyopita, al Bashir alikuwa akishikiliwa rumande "mahala salama".

Waziri mmoja wa zamani ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba al-Bashir alikuwa katika kifungo cha nyumbani katika kasri la rais ndani ya  eneo yanakopatikana makao makuu ya jeshi mjini Kahrtoum.

Sudan Proteste gegen Präsident Omar Al-Bashir in Khartoum
Baadhi ya waandamanaji mjini Khartoum Picha: picture-alliance/AP Photo

Amehamishiwa katika jela ya Kopar jana usiku. Walikuwa waasisi wa maandamano walioshinikiza al-Bashir ahamishiwe jela.

Mamia wamejiunga na madaktari na watumishi wa sekta ya afya wanaopiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi yaliyogeuka kitovu cha maandamano ya umma nchini Sudan.

Wengi wao wamevalia makoti meupe na kupepea bendera ya Sudan na kuhanikiza wakisema "uhuru, amani, haki na mapinduzi ndio matakwa ya wananchi."

Jumuia ya wasomi nchini Sudan iliyoko nyuma ya maandamano hayo imelitaka baraza la kijeshi likabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia itakayotawala kwa kipindi cha miaka minne.

Uganda inaweza kumpatia al-Bashir hifadhi ya ukimbizi akitaka.

Wakati huo huo naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uganda Henry Okello Oryem amesema "Uganda inaweza kumpatia al-Bashir hifadhi ya ukimbizi akitaka. Oryem ambae hakuzungumzia kisa cha kuwekwa rumande al-Bashir amesema tu rais huyo aliyepinduliwa ametoa mchango mkubwa katika kupatikana amani katika nchi jirani ya Sudan Kusini.

zum Thema - Friedensvertrag mit der M23 geplatzt - Kongo
Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uganda Henry Okello OryemPicha: picture-alliance/dpa

Kwa miaka kadhaa Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliyeingia madarakani mwaka 1986 hakuwa na uhusiano mzuri pamoja na al-Bashir aliyekuwa akituhumiwa kuwaunga mkono waasi wanaoipinga serikali yake.Viongozi hao wawili wamesuluhisha tofauti zao baada ya Sudan Kusini kujipatia uhuru.

Kwa upande wao waasi wa Sudan wamesema wataweka chini silaha kwa muda wa miezi mitatu katika maeneo wanayoyadhibiti , kaskazini mwa jimbo la Blue Nile.

Abdel-Aziz Adam al Hillu, mkuu wa vuguvugu la ukombozi wa wananchi wa Sudan amesema hiyo ni ishara ya "nia njema" iliyolengwa kuwapatia nafasi wanajeshi wakabidhi kwa njia ya amani madaraka kwa raia.