1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OPCW yatuzwa tuzo ya amani ya Nobel

Mjahida 11 Oktoba 2013

Shirika la kimataifa la kudhibiti silaha za sumu OPCW limesema zawadi ya zaidi ya dola milioni moja inayotolewa kwa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel itatumika kwa juhudi zaidi za kuangamiza silaha za nyuklia duniani.

https://p.dw.com/p/19yIM
Mkuu wa shirika la OPCW, Ahmet Uzumcu.
Mkuu wa shirika la OPCW, Ahmet Uzumcu.Picha: Reuters

Akizungumza katika mkutano wa vyombo vya habari mkuu wa shirika la OPCW, Ahmet Uzumcu, amesema anatarajia kupokea rasmi tuzo hiyo inayoonesha ujuzi wa wafanyakazi wake na uungwaji mkono mkubwa wanaopata kutoka kwa wanachama 189 wa shirika hilo.

Uzumcu amesema zawadi nono inayojumuishwa katika tuzo hiyo ya kitita cha dola milioni 1.25 itatumika katika kuendeleza juhudi za kuangamiza silaha za sumu.

Amesema tuzo hii inapaswa kuipa moyo dunia kuzuia mashambulizi ya silaha hizo hatari akitoa mfano wa shambulizi lililofanyika nchini Syria Agosti 21 mwaka huu.

Jengo la Makao makuu ya OPCW
Jengo la Makao makuu ya OPCWPicha: picture-alliance/dpa

Mkuu huyo amesema anatumai kuwa tuzo hiyo itafanikiwa kuleta amani nchini humo.

"Natumai kuwa tuzo hii na juhudi za shirika la OPCW pamoja na Umoja wa Mataifa itasaidia katika juhudi za kutafuta amani Syria na kusimamisha maafa wanayopitia watu wake", Alisema Ahmet Uzumcu.

Hata hivyo msemaji wa muungano wa kitaifa wa Syria, Khaleed Saleh amesema amani haiwezi kupatikana kwa ajili ya tuzo hiyo.

Ujerumani yazungumzia tuzo

Hisia tofauti zinaendelea kutolewa juu ya tuzo hiyo. Ujerumani kupitia waziri wake wa mambo ya nchi za nje, Guido Westerwelle, imesema hii ni hatua moja kubwa itakayowapa moyo watu wanaopigania kuangamizwa kwa silaha hizo hatari duniani.

Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, amesema anatumai tuzo hiyo itazidisha juhudi za shirika la OPCW katika kuangamiza silaha hizo.

Kwa upande mwengine barani Afrika, waathiriwa wa ubakaji katika hospitali ya daktari Denis Mukwege, raia wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, wamevunjwa moyo baada ya kugundua kuwa daktari huyo hakutunukiwa tuzo hiyo kama ilivyotarajiwa.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: picture-alliance/dpa/Maurizio Gambarini

Hata hivyo daktari Mukwenge, muanzilishi wa hospitali hiyo inayopokea wanawake 3,500 wanaobakwa nchini humo, amesema kupitia mtandao wake wa twitter kwamba anatoa shukrani kwa wale wote wanaomuunga mkono na kusema bado ataendelea na juhudi za kumaliza unyanyasaji wa kingono katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mwengine aliyetarajiwa kushinda tuzo hiyo ni Mwanaharakati wa elimu, msichana wa miaka 16 Malala Yousafzai, aliyepigwa risasi kichwani na waasi wa Taliban nchini Pakistan.

Msemaji wa waasi hao, Shahidullah Shahid, amesema wamefurahi kuwa Malala hakushinda tuzo hiyo kwa kuwa hakuna alichokifanya katika kuleta amani duniani.

Mwandishi Amina Abubakar/dpa/AFP

Mhariri Josephat Charo